January Makamba Abaki njia Panda Baada ya Watu Aliowafukuza Kazi NEMC Kurudishwa Kazini Kinyemela

Maswali mazito yameibuka juu ya uamuzi wa Serikali kuwarudisha kazini kimyakimya wajumbe saba wa bodi na watendaji waandamizi wanne wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), siku chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, kuwasimamisha.

Mwananchi limedokezwa kuwa hivi sasa watumishi hao, akiwamo Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Vedasto Makota wanaendelea na kazi zao kama kawaida kwa maelekezo ya mamlaka za juu.

Wiki mbili zilizopita, Makamba alitangaza kutengua uteuzi wa wajumbe saba wa Bodi ya NEMC na kuwasimamisha wakurugenzi wake wanne ---Manchare Heche, Deus Katwale, Andrew Kalua na Benjamin Dotto--- kwa tuhuma kadhaa ikiwamo ya ucheleweshaji wa vibali vya ukaguzi wa mazingira na tuhuma za rushwa.

Alisema NEMC ina upungufu mkubwa kiutendaji huku akiwatuhumu baadhi ya watendaji kwa kuwasaidia watu wenye masilahi nao na kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha pale walipotakiwa kufanya hivyo.

“Kulingana na mamlaka niliyonayo chini ya Sheria ya Mazingira Kifungu cha 19 (2), nimeamua leo kutengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye niteue wajumbe wapya ambao wataenda na kasi na ari tunayoihitaji sasa katika kuelekea uchumi wa viwanda. Mwenyekiti wa Bodi, ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni Mheshimiwa Rais, ataendelea kuwepo hadi Mheshimiwa Rais atakapoteua mwingine.”

Pia alisema, “Tumewasimamisha kazi baadhi ya watendaji wa NEMC kuruhusu uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili kabla ya kuchukua hatua zaidi.”

Makamba alimteua Dk Elikana Kalumanga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC.

Hata hivyo, baada ya hatua hiyo, imeelezwa kwamba wote walioondolewa wamerejeshwa kimyakimya. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Vedasto Makota hakupatikana kuzungumzia suala hili na mmoja wa waliosimamishwa kazi, Heche hakukataa wala kukubali kwamba amerudishwa kazini, akisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa liko chini ya mamlaka ya waziri.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa tangazo hilo la Makamba halikudumu kwa zaidi ya wiki moja baada ya mamlaka za juu kuagiza hali irudi kama ilivyokuwa awali.

Baadhi ya watu walio ndani ya NEMC wamedai kuwa uamuzi huo wa Serikali utaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa Baraza hilo la Mazingira linalokabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha mchango wake katika masuala ya uhifadhi wa mazingira kuhojiwa mara kwa mara.

“Hapa palishageuka kama himaya ya watu fulani tu. Hakuna kinachoenda. Malalamiko ni mengi kutoka jumuiya ya wafanyabiashara na wenye viwanda. Sio siri tena kwamba rushwa imetawala hasa katika eneo la utoaji vibali vya mazingira,” alisema ofisa mmoja wa daraja kati wa NEMC kwa sharti la kutotajwa jina.

“Kuna ukiritimba mkubwa kutoa cheti cha mazingira na mtu kama akiwa tayari kutoa pesa anapata hata ndani ya siku mbili tu. Kama huna utasumbuka sana,” alisema ofisa huyo.

Wizara ya Viwanda na Biashara imewahi kusikika mara kadhaa ikilalamikia ucheleweshaji wa utoaji wa vibali vya mazingira kama moja ya mambo yaliyozorotesha jitihada za Serikali za ujenzi wa viwanda nchini.

Akiwa katika ziara ya kikazi Mkoa wa Pwani mwezi uliopita, Rais John Magufuli alionyesha waziwazi kukerwa na ucheleweshaji wa vibali vya mazingira unaofanywa na NEMC na alizungumzia suala hilo mara mbili katika mikutano yake ya hadhara.

Mbali na ucheleweshaji wa vibali vya mazingira, rushwa inatajwa kukithiri ndani ya wakala huyo wa mazingira huku watendaji wakidaiwa kuwatoza faini wenye viwanda kinyume cha sheria na wakati mwingine kuwatisha ili watoe rushwa kwa ahadi ya kuwapunguzia faini.

Akitoa mfano, ofisa mwingine wa NEMC aliyeomba kutotajwa jina amesema baadhi ya maofisa waliwahi kukitoza kiwanda cha kuchinja nyama ya punda mjini Dodoma kinachomilikiwa na raia wa China faini ya Sh240 milioni kinyume na Sheria za Mazingira.

Suala hilo linadaiwa kufika mezani kwa waziri Makamba ambaye baada ya uchunguzi na kuweka vielelezo mezani zikiwamo risiti za tozo, ikagundulika wawekezaji hao walilipa Sh20 milioni tu huku watu wa NEMC wakiondoka na Sh100 milioni baada ya kukubali kuwapunguzia Wachina hao kiasi cha faini.

Ofisa huyo alidai kuwa watendaji hao waliamua kughushi mukhtasari kuonyesha kwamba mwekezaji huyo aliomba kupunguziwa faini.

Taarifa zinasema kuwa watendaji wote wa NEMC waliotajwa kwenye mukhtasari huo baada ya kubanwa walikikiri kuwa hawakuhudhuria mkutano uliozaa mukhtasari huo na kwamba hawana mamlaka ya kumpunguzia mtu faini isipokuwa waziri peke yake.

Mtoa taarifa wetu anadokeza kuwa hata bodi ilipofikishiwa suala hili ikasema watu hao wapewe onyo wakati kosa ni la wazi kabisa.

“Huku ni kulindana tu na NEMC isipokuwa overhauled (fumuliwa) tusitegemee chochote. Hizi ni zama za accountability (uwajibikaji) na kwa kweli kuna mambo hayaendi sawa humu mwetu. Sisi tukiboronga madhara kwa nchi ni makubwa kuliko watu wanavyoona,” alisema ofisa huyo wa NEMC.

Alipotafutwa kwa simu, waziri Makamba alikataa katakata kuzungumzia suala hilo. “Sisi tuko vizuri tu na tunatekeleza mipango ya Serikali kama kawaida. Sina zaidi ya hilo,” alisema.

Habari kutoka ndani ya wizara zinasema kukithiri kwa matatizo ndani ya NEMC kuliwahi kumsukuma Waziri Makamba kuwaita watendaji wake na kuandaa mkakati wa kuyashughulikia, wakilenga zaidi suala la utoaji vibali vya mazingira kwa kuangilia muda unaotumika kwa kazi hiyo, gharama na kuziba mianya yote ya rushwa.

Vyanzo vyetu vinasema kuna wakurugenzi ambao wanakabiliwa na tuhuma za wazi za kukiuka sheria za utumishi wa umma ikiwamo rushwa na ndizo zilizomsukuma Waziri Makamba kuwasimamisha kazi akijipanga kufanya mabadiliko makubwa ndani ya NEMC.

Watu wanaofuatilia kwa karibu sakata hili wanasema makundi yenye masilahi ya kiuchumi na NEMC hawakupendezwa na mwelekeo wa Makamba katika kuifumua NEMC ndipo wakaanza mkakati wa chini kwa chini kukabiliana naye.

Makundi hayo ndiyo yanayodaiwa kuiteka NEMC na yanalaumiwa kwa kukwamisha juhudi mbalimbali za wizara na Serikali kwa miaka mingi sasa kama vile kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki na kudhibiti viwanda dhidi ya uchafuzi wa mazingira na kujenga jumba za kifahari ndani ya hifadhi za fukwe mbalimbali.

Haijulikani ni nani, katika mazingira gani na kwa sababu ipi aliamuriwa ‘kumzima’ Waziri Makamba lakini vyanzo vyetu ndani ya NEMC vinaonya kuwa uamuzi huo utaadhiri utendaji kazi wa baraza na kumpunguzia waziri mamlaka ya kiutawala dhidi ya Baraza hilo.

Habari zinasema tayari Wangwe, alikwishapewa barua ya kuondolewa NEMC na kurudishwa Hazina.

Wafuatiliaji wanahoji pia ni jinsi gani Makamba atapeleka uso wake na kuanza kufanya kazi na kundi la watu ambao hana imani nao tena na alikwishaamua kuwaondoa kazini.

“Huu uamuzi sijui umechukuliwa na nani lakini jambo lililo wazi ni kwamba utamuondolea kabisa waziri moral authority (mamlaka ya kimaadili) kutimiza mipango yake na watu hawa waliorudishwa. Hali hii nina hakika imemshushia hadhi hapo wizarani na itakuwa imemvunja sana moyo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Wadadisi pia wanahoji endapo mikakati iliyopo ya kuifumua NEMC na kuifanya ifanye kazi kwa ufanisi na uadilifu zaidi itatekelezwa katika mazingira ya sasa.

Kwa upande mwingine, suala hili kwa namna moja au nyingine limeiweka majaribuni vita ya Rais Magufuli dhidi ya rushwa na utendaji usioendana na kasi yake hasa ikizingatiwa hata aliwahi kuonyesha kutoridhishwa na ufanisi wa NEMC.

“Tatizo ni wazi kabisa hawa watu walishafeli kabisa katika majukumu na Makamba aliona ili mambo yaende lazima awaondoe. Sasa changamoto kwa huyu bwana (Makamba) ni kuhakikisha kazi na mipango yake vinaendelea katika hali ya vikwazo vilivyo mbele yake,” anasema.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema inawezekana waziri huyo kijana hakufanya mawasiliano ya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi wake.

“Hili haina tafsiri nzuri. Nchi nyingine waziri huwa anajiuzulu kwa sababu mamlaka yake yamevizwa. Inawezekana alichukua hatua hiyo bila mawasiliano ya kutosha. Sidhani kama walimpa go ahead (ruhusa) halafu wa-reverse (wageuke),” anasema Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala.

“Unajua mfumo wa utawala wetu wa sasa walio chini ya Rais mara nyingi wanachukua hatua kwa kudhani wanampendeza Rais au waonekane wanafanya kazi lakini si mara zote hiyo inafanya kazi.”

Profesa wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana alisema hatua ya Serikali kubadili uamuzi ya Makamba inaashiria kuwa hakufanya mawasiliano ya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi wake.

“Nafikiri inawezekana ni tatizo la mawasiliano na mamlaka. Unajua kimsingi Makamu wa Rais ndiye mwenye dhamana. Waziri hana instruments. (mamlaka). Sasa kuvunja bodi ni dhamana ya Makamu wa Rais. Swali kubwa la kujiuliza hapa ni je, Makamu wa Rais alijulishwa na kuridhia mpango wa Makamba? Kama hakuridhia inawezekana ndiyo sababu mambo yamekuwa hivyo,” alisema Bana.

Source: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad