Mwanamuziki Tom Mboya Ang’ang’a, anayejulikana kwa jina la kimuziki kama Atomy Sifa aliyekimbia nchi yake ya Kenya baada ya wafuasi wa mwanasiasa wa upinzani nchini humo, Raila Odinga kuanza kumsaka kwa kutaka kumuua baada ya kumdharaulisha shujaa huyo wa Kabila la Wajaluo kwenye moja ya nyimbo zake.
Atomy Sifa akishirikiana na Tede ja Kenya waliandika wimbo uliomsifu mgombea wa chama tawala nchini Kenya – Uhuru Kenyatta, kwenye wimbo ujulikanao kama ‘Uhuru Nyale’ (Uhuru anaweza) ambao ndani yake pia amemponda mwanasiasa wa Muungano wa Vyama vya Upinzani wa NASA, Raila Odinga na kuwataka watu wa kabila la Luo kuacha kumfatafata.
Baada ya wimbo huu, ilimlazimu mwanamuziki Sifa akimbilie nchini Tanzania baada ya kupokea vitisho kutoka kwa watu kadhaa waliokuwa wakimlaumu kwa kumfanya Raila aonekane mbaya na kudhalilisha kabila la Wajaluo.
Baada ya kuanza kwa matukio hayo, Atomy alisema kuwa alishawishiwa na mwanamuziki mwenzake kutunga wimbo wa kumfanya Raila Odinga aonekane si lolote na akasema wakati wanatunga wimbo huo, hakujua kama utakuja kutumika sehemu yoyote, hasa kwenye kampeni.
“Sikujua wimbo wenyewe unaohusu nini. Nilialikwa nishiriki kutokea kwenye video ya wimbo huo lakini baadaye ndio nilipojua kuwa lengo la wimbo wenyewe lilikuwa kumdhalilisha Bwana Raila Odinga. Kwakweli sikujua wimbo huo kama utatumiwa,” alisema Atomy Sifa.
Kituo cha habari nchini humo, The Daily Nation kimesema kwamba kina uthibitisho wa sababu za kutungwa na kurekodiwa kwa wimbo huo wakisema kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ya Kenya (NIS) iliwalipa Atomy Sifa na Tede ja Kenya kutunga wimbo wa kumdhihaki Raila Odinga baada ya kushindwa kuwarubuni wanamuziki wengine wengi wa kabila la Luo (ambalo ndio kabila la mwanamuziki huyo).
Wameripoti kuwa Idara ya Usalama wa Taifa iliwafata wasanii wengine wawili wa kabila la Wajaluo ambao walikutana katika hoteli ya Choma Zone lakini hawakufikia muafaka kuhusu malipo kwa sababu walitaka kiasi kikubwa cha fedha.
Sifa, ambaye alikuwepo kwenye mkutano wa kwanza alikubali kurekodi wimbo huo wa kumponda Raila Odinga baada ya kukutana kwa mara ya pili na maafisa usalama baada ya mkutano wa kwanza kutokuwa na matunda yoyote.
The Daily Nation wamesema kwamba mwanamuziki huyo alitaka kiasi kidogo cha pesa, kidogo zaidi ya kile kilichoombwa na wenzake – jambo lililofanya maafisa hao kulipa kirahisi kisha kumpatia msanii huyo mkataba ambao alitakiwa kusaini kabla hajapewa pesa aliyotaka. Baada ya hapo alipatiwa mashairi yaliyokuwa yameshaandaliwa na alitakiwa kuyaimba kama yalivyo bila kubadili chochote.
Baada ya hapo, video ya wimbo huo iliandaliwa na kuwekwa kwenye mtandao wa YouTube na maafisa hao kisha wafuasi wa Jubilee kuisambaza kwa kasi.
Joto la Uchaguzi Kenya...Mwanamuziki Akimbilia Tanzania Baada ya Kumtukana Mgombea Urais
0
August 01, 2017
Tags