Kamanda Mkondya Aanza na Kibarua Kigumu Atakiwa Kuwakamata Vigogo Bodi ya Korosho

Kamanda Mkondya Aanza na Kibarua Kigumu Atakiwa Kuwakamata Vigogo Bodi ya Korosho
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Naibu Kamishna Lucas Mkondya, ameanza kazi katika kituo chake hicho kipya kwa kibarua kizito cha kutakiwa kuwakamata vigogo wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) wanaotuhumiwa kusambaza pembejeo zilizopita muda wa matumizi.

DCP Mkondya ambaye kabla ya kwenda Mtwara alikuwa Kaimu kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, ameagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, kuwakamata vigogo hao, akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Hassan Jarufu.

Dengego aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa, amepokea taarifa kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kuhusu kuwapo kwa dawa za kuua wadudu kwenye mikorosho ambazo zimekwisha muda wa matumizi kwa ajili ya kupelekwa kwa wakulima wa zao hilo katika msimu wa mwaka 2017/18.

Baada ya kupata habari hizo, alifanya ziara fupi kwenye ghala la viuatilifu la Mtwara na kugundua kuna dawa za maji zaidi ya lita 400 zilizokwisha muda wake na zikiwa na vifungashio vyenye majina tofauti na dawa zilizomo ndani.

Vifungashio hivyo vimeonyesha kuwa dawa hizo zilitengenezwa mwaka 2017 huku dawa zilizomo ndani ambazo pia muda wake wa matumizi umeisha zikionyesha kutengenezwa mwaka 2012.

Vigogo wengine wanaotakiwa kukamatwa kwa amri ya Dengego ni Meneja Rasilimali Watu wa Bodi hiyo, Shauri Mokiwa, Mkurugenzi wa Kilimo na Ubanguaji, Luseshelo Silomba na mkurugenzi wa kampuni inayohusika na ulinzi wa ghala hilo.

"Serikali ya mkoa imesikitishwa sana na jambo hili ambalo limeendelea kufanywa na watendaji wa Bodi ya Korosho. Ofisi yangu haitafumbia macho jambo lolote litakaloonekana kutia doa azma ya serikali kuwainua wakulima," alisema Dendego.

Wakati Dendego akitoa amri hiyo, Kamanda Mkondya alisema hadi jana mchana jeshi lake lilikuwa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma hizo.

Aliwataja watu haio kuwa ni Felista Onestina ambaye ni mtunza ghala na katibu mahususi wa Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Emiliana Salia na Husna Rajabu wote wakiwa watunza ghala.

"Bado tunaendelea na ufuatiliaji wa tukio hili hadi ngazi za juu ili kuhakikisha watuhumiwa hawa tunawakamata kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi," alisema Mkondya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad