Rais Uhuru Kenyatta huenda akaingia katika vitabu vya kumbukumbu na historia kwa marais wa Afrika kwa kuamua kuruhusu maandamano ya amani kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Kenyatta amewataka polisi kujizuia kutumia nguvu kubwa na badala yake wawape ulinzi wakati wa maandamano hayo ya amani na yanayoruhusiwa kisheria kwa watu ambao hawafurahii matokeo ya uchaguzi uliopita.
Rais Kenyatta alisema hayo jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa wagombea walioshindwa katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne iliyopita.
Kenyatta alisema hayo akiwa Jengo la Harambee alikokwenda kukutana na Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya kuapishwa kwake.
Katika ujumbe huo uliomlenga zaidi Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Nasa, Kenyatta aliwataka wagombea wote ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi wachukue hatua zilizobainishwa na Katiba ili kupata wanachotaka.
“Marafiki zetu ambao hawataki kukubaliana na matokeo … tumenyosha mkono wetu wa udugu kwao … watumie njia zozote zilizobainishwa katika katiba kuelezea kutoridhishwa kwao,” alisema.
“Wale wanaotaka kushawishi wengi wagome wanaweza kufanya hivyo, lakini kwa kuzingatia vifungu vya sheria. Mwishoni mwa siku sisi sote ni Wakenya. Hakuna haja ya kudhuriana. Hakuna haja ya kuharibiana mali…tunawashukuru polisi kwa kazi nzuri lakini waendelee kujizuia.”
“Polisi wako tayari kuwalinda wakati mnafanya maandamano na wale waliochukia waelewe kwamba hawahitaji kibali changu wala cha Jubilee kufanya maandamano ya amani.”
Hata hivyo, alitoa onyo kali kwamba serikali haitavumilia maandamano yatakayosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu kutokana na vurugu.
Vilevile alitoa onyo dhidi ya waporaji na waharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo ya nchi, ambako yameripotiwa maandamano baada ya uchaguzi.
“Wakenya wengi wamesema uchaguzi umepita na wamerejea kazini. Hawataki maandamano ya ghasia. Msivuruge maisha ya watu wengine. Kama serikali hatutaruhusu uharibifu wa mali wala upotevu wa maisha na uporaji.”
Rais Uhuru alitoa kauli hiyo baada ya viongozi wa muungano wa Nasa kuhamasisha wafuasi wao kukataa matokeo yaliyompa ushindi Uhuru na makamu wake, William Ruto.
Baada ya kazi ya kuhesabu kura kukamilika, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi kwa kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27.
IEBC ilisema mgombea urais kwa muungano wa Nasa, Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 matokeo ambayo wanayapinga.
Wakiitikia wito wa viongozi wao kati ya Jumatano na Jumamosi maeneo, ambayo ni ngome ya upinzani ya Kisumu, Kibera, Homabay na Migori yalikumbwa na vurugu na soko la Garissa lilichomwa moto.
Nasa walidai kwamba, kwa mujibu wa vyanzo vyao kutoka ndani ya IEBC Raila alishinda kwa kura milioni nane akifuatiwa na Uhuru. Walidai wizi huo ulifanikishwa kwa kudukua kompyuta iliyokuwa inahifadhi matokeo na kumbukumbu nyingine.
Juzi, akizungumza na wafuasi wake waliojitokeza kwa wingi katika eneo la Kibera, Raila aliwataka wafuasi wake wote kususia kazi jana ili kuomboleza vifo vya waliouawa katika makabiliano na polisi.Pia, alisema atatoa msimamo leo wa nini cha kufanya.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kutii wito wa serikali, watu walionekana kupuuza wito wa Raila wa kususia kazi kuomboleza watu waliouawa katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
Wengi walionekana barabarani wakirejea kwenye shughuli zao jana na kuendelea na maisha ya kawaida.