Kimenuka...Aliyeisaliti CCM Kwenye Uchaguzi Kujadiliwa na Kamati ya Maadili


Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini inatarajiwa kukutana na kujadili hatua ya Diwani wa Kata ya Sunguti, Denis Ekwabi kukisaliti chama hicho na kumpigia kura mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati wa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti uliofanyika katika Halmashauri ya Musoma Vijijini.

“Sisi baada ya uchaguzi kuisha tuliitana wanachama wote wa CCM ili kutaka kujua nani aliyetusaliti wakati kwenye vikao vyetu vya ndani ya chama tulikuwa tumeshampitisha mgombea wetu atakayegombea nafasi hiyo na tukakubaliana, lakini tulipokutana tu Diwani wa Kata ya Sunguti, Denis Ekwabi alikiri mwenyewe kuwa ndiye aliyepigia kura CHADEMA,” alieleza Bernard Ghati, Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini

Katibu huyo alilaani kitendo cha Diwani huyo kukisaliti chama na kupigia kura chama kingine, akieleza kuwa ni utovu wa nidhamu na kutozingatia kanuni za chama hicho, hivyo watakapokutana na Kamati ya Maadili watatoa tamko juu ya tukio hilo.

Ghati alisema kuwa idadi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo ni 26 na Madiwani wa CCM wapo 22 na wa CHADEMA wanne, lakini kura zilipopigwa zilionesha kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti kupitia CHADEMA alipata kura tano na wa CCM alipata kura 21, kitendo kilichowafanya wanaCCM kubaini kuwa kuna mmoja wao aliyewasaliti.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad