Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea kulia na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kutokana na kile alichodai ni hujuma anazozifanya dhidi ya chama hicho akishirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba.
Maalim Seif alieleza hayo juzi katika barua yake ya kumjibu Jaji Mutungi kuhusu hatua yake ya kuwatambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF na Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu wakati viongozi hao walisimamishwa uanachama kwa tuhuma mbalimbali.
Katibu mkuu huyo alifikia uamuzi wa kumjibu Jaji Mutungi baada ya ombi lake la kuwafukuza uanachama wabunge wawili; Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kugonga mwamba kutokana na msajili kumtambua Sakaya kama kaimu katibu mkuu kufutia maelezo aliyopewa na Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba alimweleza Msajili kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutofika ofisi ya chama hicho zilizopo Buguruni, hivyo akamteua Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara kukaimu ukatibu mkuu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CUF mimi, Maalim Seif bado ni katibu mkuu wa chama hiki na nipo hapa nchini, ni mzima na nina akili timamu. Na nafasi yangu haiwezi kukaimiwa na Sakaya ambaye tulishamsimamisha uanachama,” inaeleza barua hiyo.
“Mheshimiwa msajili, nashangaa kwa maelezo yako. Mimi ninavyojua ni kuwa kiongozi anakaimiwa ikiwa hayupo nchini au hawezi kutekeleza majukumu yake. Hivyo ndivyo katiba ya CUF ya 1992 (toleo la 2014) kifungu cha 105 (1) kinavyoeleza.”
Aliongeza kuwa Jaji Mutungi alipokea barua ya Profesa Lipumba Machi 16, 2017 huku yeye akiwa hapa nchini akiendelea na shughuli za chama hasa katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Zanzibar kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Maalim Seif alisema cha kushangaza Msajili wa Vyama vya Siasa alitoa uamuzi kutokana na maelezo ya mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi yake. Kutokana na hilo, mwanasiasa huyo alimtaka Jaji Mutungi kuangalia katiba ya CUF ya mwaka 1992 (toleo la 2014) kifungu Na. 1 (2) vinavyoeleza kwamba makao makuu ya chama hicho yatakuwa katika Mji Mkuu wa Zanzibar na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Alisema kifungu cha 1 (3) kinaeleza kwamba kutakuwa na Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya Chama Dar es Salaam na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
“Kwa mantiki hii, Mheshimiwa Jaji Mutungi wewe mwenyewe umeshawahi kuyatembelea makao makuu hayo au bado ofisi iliyopo Buguruni, Dar es Salaam ndiyo Ofisi Kuu ya Makao Makuu?” inahoji barua ya hiyo. Maalim Seif ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema kesi mbalimbali zinazohusu mgogoro wa CUF zimefunguliwa Mahakama Kuu na kwamba, ni vyema Jaji Mutungi angetumia busara kumweleza Profesa Lipumba asubiri hukumu ya mahakama na endapo angekataa msajili na ofisi yake ingejitenga naye.
Mbali na hilo, Maalim Seif alidai kwamba msajili katika barua yake alieleza kwamba amejiridhisha na maelezo ya Profesa Lipumba kuwa yeye hafiki Buguruni na ameshindwa kufanya kazi, lakini hakumtafuta au kumuita ama kumuuliza ili kupata maelezo yake kujua ukweli wa kilichoandikwa na mwenyekiti anayemtambua.
Mwananchi:
MAALIM Seif Aendelea Kula Sahani Moja na Msajili wa Vyama Vingi, Amlima Barua Kali
0
August 20, 2017
Tags