Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaka mabango yanayoonyeshwa na wananchi kwa viongozi wa kitaifa wanapowatembelea yasiwe yanazuiwa kwa vile yanakuwa yanaelezea changamoto wanazokabiliana nazo.
Majaliwa alisema hayo baada ya kuona mabango yaliyoinuliwa na wananchi kwenye mkutano wake na wananchi mwishoni mwa juma lililopita mjini Sikonge mkoani Tabora huku wananchi hao wakitakiwa kuyashusha.
“Siku nyingine msirudie na kuanzia sasa waacheni wananchi waonyeshe mabango yao kwani ndiyo njia wanayotumia kuonyesha hisia zao kwa yale wanayokumbana nayo na kuwasababishia kero,” alisema Majaliwa.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wasaidizi wake wayakusanye mabango yote wayaandike kisha wampelekee yaliyomo akiahidi kwamba atayafanyia kazi.
Alieleza kuwa malalamiko mengi kwenye mabango hayo yanahusu kero za vyama vya msingi vya ushirika na migogoro ya ardhi na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kutenga siku kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi huku akiwa na wakuu wa idara mbalimbali.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa wananchi kuinua mabango kwa viongozi wa kitaifa. Julai 22 huko Kigoma wakati wa ziara ya Rais John Magufuli, wananchi waliinua mabango yao ili ayasome huku wakizuiwa na walinzi.
“Waacheni, waacheni tu jamani…jamani mtulie nitayasoma yote. Nimeyaona yote ndiyo maana nayapitia na wasaidizi wangu wanayapiga picha nyinyi msiwe na wasiwasi,” alisema Rais Magufuli wakati akihutubia katika Uwanja wa Lake Tanganyika huku wananchi wakikazana kumwonyesha mabango yao.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena huko Tabora Julai 23, wakati Rais Magufuli akiwahutubia wananchi na kuwataka washushe mabango yao kwa sababu wananchi walikuwa wakipiga kelele, jambo lililokatisha hotuba yake.
“Naomba myashushe mabango yenu ili niendelee na hotuba yangu,” alisema Rais Magufuli lakini wananchi waliendelea kuyainua juu, jambo lililoonyesha kumkera, “Nimesema shusheni hayo mabango, la sivyo siyashughulikii. Ukitaka hata ukayatandike kwenye kitanda cha mke wako, siyasomi.”
Akitoa maoni yake kuhusu vitendo vya wananchi kuinua mabango yao kwa viongozi wa kitaifa, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema hiyo inaonyesha kukua kwa demokrasia nchini.
Alisema wananchi wanatafuta namna ya kufikisha ujumbe kwa viongozi wa kitaifa juu ya mambo ambayo Serikali za mitaa au mkoa zimeshindwa kukabilaiana nazo au wameshindwa namna ya kuwafikia.
“Huko ndiko kupevuka kwenyewe na kukua kwa demokrasia. Viongozi kwenye maeneo hayo wameshindwa kutatua kero za wananchi ndiyo maana wananchi wanaona bora watumie fursa ya kueleza kero zao kupitia mabango,” alisema.
Mwanazuoni huyo alisisitiza kwamba kuna haja ya kuimarisha mifumo ya mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao wa Serikali za mitaa mpaka mkoa ili kumaliza changamoto zao bila kuzifikisha kwa viongozi wa kitaifa.
“Viongozi wa mikoa wawe na mawasiliano ya karibu na wananchi, wawe wanajibu meseji zao na kuwafikia katika maeneo yao. Hiyo itasaidia kupunguza mabango kwa viongozi, japo siyo jambo baya pia kuinua mabango,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kitendo cha wananchi kuonyesha mabango kwa viongozi kinaonyesha udhaifu wa Serikali katika kukabiliana na changamoto za jamii husika.
Alisema mara nyingi askari wamekuwa wakiwazuia wananchi kupaza sauti zao ndiyo maana nao wameamua kuja na mtindo wa kutumia mabango kufikisha ujumbe kwa viongozi wao wa kitaifa. “Katiba yetu inaruhusu uhuru wa kutoa maoni bila kujali kwamba yatawafurahisha au kuwakera viongozi. Askari wasitumie nguvu kuwanyamazisha wananchi kwa sababu ni haki yao ya msingi,” alisema Muabhi.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alimpongeza Waziri Mkuu kwa kutambua umuhimu wa sauti ya umma na kusisitiza kwamba hiyo ni njia moja wapo ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Alisema siyo jambo baya kwa wananchi kuinua mabango yao kwa viongozi kwa sababu wakati mwingine wanawakumbusha juu ya mambo ambayo wanatakiwa kuyafanyia kazi.