Wakati operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizoko ndani ya umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro ikiendelea maeneo ya Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeziwekea kinga ya muda nyumba 286 zinazohusika.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa juzi na Jaji Leila Mgonya kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi hao 286 wa maeneo ya Ubungo- Maji hadi Kiluvya wakiomba itoe zuio la muda hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Maombi hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi yamepangwa kusikilizwa Agosti 30 baada ya upande wa wajibu maombi (Serikali) kuwasilisha hati ya kiapo kinzani.
Hata hivyo, wakati wakisubiri usikilizwaji wa maombi ya zuio la muda, wananchi hao kupitia kwa wakili wao, Benito Mandele waliwasilisha maombi ya dharura wakioomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Jaji Mgonya anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi hayo na kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi tarehe hiyo ya maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kwa uamuzi huo, Tanroads ambayo ndiyo mtekelezaji wa operesheni hiyo haitaweza kuzigusa nyumba hizo hadi hapo mahakama itakavyoelekeza vinginevyo baada ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio la muda kusubiri kesi ya msingi kumalizika.
Wakili Mandele alisema kuwa watakachofanya baada ya kupata hati ya amri hiyo ya mahakama wataitoa nakala nyingine na kuwagawia kila mdaiwa kwa ajili ya kuiweka kwenye nyumba yake.
Katika kesi ya msingi namba 284 ya mwaka 2017, wananchi hao wanaiomba mahakama itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo yenye mgogoro na kwamba hawapo katika hifadhi ya barabara.
Pia, wanaiomba mahakama hiyo iamuru kuwa kama Serikali inata kuwahamisha na kuyachukua maeneo yao, basi iwalipe fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Tanroads imetoa notisi kwa wakazi wote walipo katika umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara ya Morogoro kila upande, kuanzia Ubungo - Maji hadi mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani kuvunja nyumba zao kwa madai kuwa wapo kwenye hifadhi ya barabara.
Hivyo, Tanroads waliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Wananchi hao wanapinga amri hiyo wakidai kuwa wanaishi katika maeneo hayo kihalali kwa kuwa wana hatimiliki halali na hawapo kwenye hifadhi ya barabara, huku wakihoji sheria iliyotumika kuidhinisha umbali huo wa mita 121.5.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameamua kwenda mahakamani katika makundi tofauti na kufungua kesi tofautitofauti kupinga operesheni hiyo wakidai kulipwa fidia kama Serikali itawahamisha.
Mbali na kesi hiyo iliyotolewa amri hiyo, pia kuna kesi nyingine mbalimbali ambazo ziko katika hatua mbalimbali.
Kesi hizo nyingine ni ile iliyofunguliwa na Abdallah Maliki kwa niaba ya wenzake 570 ambao ni wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi na Kiluvya dhidi ya Tanroads na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa upande mwingine.
Shauri jingine ni maombi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kupinga operesheni hiyo lililofunguliwa na Ephrahim Kavishe na wenzake wanne ili wawe wawakilishi wa wenzao zaidi ya 198 ambao ni wakazi wa Kimara Stop Over na Mbezi.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mmoja wa wajibu maombi hayo amewawekea pingamizi akiiomba mahakama hiyo iyatupile mbali maombi hayo huku akiainisha kasoro mbalimbali za kisheria.
Maombi hayo yanasikilizwa na Jaji Crencecia Makuru na amepanga kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya maombi hayo kama yataendelea kusikilizwa au yatatupiliwa mbali.