Mahakama imetoa amri ya Jengo la Klabu ya Yanga lililopo mitaa ya Jangwani kunadiwa.
Hii inatokana na deni la kodi ya Majengo la Sh milioni 360 ambazo klabu hiyo inadaiwa na Serikali.
Siku ya mnada imepangwa kuwa Agosti 19 yaani keshokutwa kuanzia saa 4 asubuhi na Msolopa Investment ndiyo itakayohusika na mnada huo.
Hali hiyo inaonekana kuwashitua mashabiki wengi wa Yanga.
Mtandao huu ulifanya juhudi za kumtafuta msemaji wa Yanga Dismas Ten, simu yake iliita bila kupokelewa ndipo alipotafutwa msaidizi wake, Godlisten Anderson Chicharito na kusema yeye hafahamu chochote na atafutwe katibu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa ndio mwenye majibu ya madai hayo.
Hata hivyo, baadaye Kampuni ya Msolopa kupitia kwa mkurugenzi wake, Ibrahim Msolopa, ilitangaza kuahirisha kwa mnada huo kutokana na makosa yaliyofanyika kabla ya kutoka kwa tangazo hilo kwani walipanga mnada huo ufanyike leo na sio Jumamosi kama ambavyo tangazo linavyosomeka magazetini.