Maswali 7 Aliyojibu Mkemia Kuhusu Mkojo wa Manji Mahakamani leo

Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dominician Dominic leo August 23, 2017 ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu matokeo ya uchunguzi wa mkojo wa Mfanyabiashara Yusuph Manji, kuwa yalionesha alikutwa na kemikali aina ya benzodiazepines na morphine.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, Shahidi huyo alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa Februari 9, 2017 saa 5 asubuhi alipokea Askari akiwa na watuhumiwa wawili kwa ajili ya kutoa sampuli ili kupima mkojo.

1: Wakili Vitalis: Je, unakumbuka watuhumiwa kwa majina yao na Askari aliyewaleta?

Mkemia: Ndio, watuhumiwa waliofikishwa ofisini hapo ni Mchungaji Gwajima na Manji ambao waliletwa na Koplo Sospeter mwenye namba E 1135.

2: Wakili: Jinsi gani ulianza kufanya uchunguzi?

Mkemia: Kuna maliwato maalum ambayo askari anaingia na mtuhumiwa kutoa sampuli ambapo nilimpatia kontena niliyoipa namba ya maabara 367/2017 ambayo sampuli hii ilikuwa ya Manji.

3: Wakili: Je, kuna chochote kiliwasilishwa kwako na nani aliwasilisha fomu namba 001?

Mkemia: Sampuli iliwasilishwa na fomu maalum kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya ambayo Koplo Sospeter ndiye aliyeiwasilisha.

4: Wakili: Je, ukiiona fomu hiyo utaweza kuitambua? Pia uieleze Mahakama baada ya kuchukua sampuli ya mkojo ulifanya nini?

Mkemia: Fomu hiyo naweza kuitambua kwa kuwa ina saini yangu na jina la Mtuhumiwa aliyeletwa kwa ajili ya uchunguzi.

“Nilifanya uchunguzi wa awali kwa kutumika kifaa kinachoitwa Diaquicky multpanel urine test na matokeo yalionesha kuwa mkojo ulikuwa na kemikali inayoitwa benzodiazepines.

Kuwepo kwa dawa hizi wakati mwingine hutumika kupunguza maumivu na matumizi mengine kulingana na daktari anavyosema.”

5: Wakili: Baada ya hatua ya kwanza ulifanya nini kwa hatua ya pili kuthibitisha dawa hizo?

Mkemia: Kemikali hizi zipo za aina nyingi lakini ili kupata majibu kama kweli anatumia dawa za kulevya nilichukua kemikali hiyo na kuunganisha na dawa za kulevya kulinganisha. Katika sampuli hii niligundua kwamba mkojo una kemikali aina ya morphine.

Alidai kemikali hiyo ya Morpine ilikuwa ndani yake na chembechembe ya dawa za kulevya aina ya heroin. Dawa hii pia hutumika hata wakati wa upasuaji mahospitalini.

6: Akiulizwa maswali na Wakili wa utetezi Ndusyepo alihoji shahidi kueleza kama mkojo ni wa Manji au Polisi?

Mkemia: Sijui kama Mkojo ni wa Manji au Polisi kwa sababu sikwenda nao maliwato wakati wa kutoa sampuli ila nililetewa sampuli na Polisi, nilikuwa nje.

7: Wakili Ndusyepo; ulitumia sampuli kiasi gani kufanya uchunguzi hatua ya pili?

Mkemia; Sampuli inayohitajika ni ujazo wa milimita 10.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad