Matibabu wanafunzi wa Lucky Vincent Ambao Wanatarajia Kuwasili Leo ni sawa na Sh 1.7bilioni
0
August 18, 2017
Maisha yana thamani kuliko kitu chochote, ndivyo unavyoweza kusema. Wanafunzi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini hapa waliopelekwa nchini Marekani kwa matibabu kutokana na kupata ajali mbaya wanarejea leo nchini huku matibabu yao ‘yakigharimu’ Sh1.7 bilioni.
Wanafunzi hao ni Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo walionusurika katika ajali ya gari iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja. Watawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) leo saa tatu asubuhi baaada ya kuondoka Marekani jana saa 9:00 mchana.
Akizungumzia kuhusu ujio wa watoto hao jana, Mbunge wa Singida Kaskazini ambaye pia ni mwenyekiti mweza wa Shirika la Stemm, Lazaro Nyalandu alisema tayari wameondoka Marekani na matibabu na gharama nyingine zikiwamo za usafiri ni zaidi ya Dola 800,000 za Marekani (Sh1.7 bilioni).
“Gharama iliyotumika ni kubwa ila hakuna fedha iliyotolewa kwa sababu kila hatua iliyohitaji malipo wahusika walijitolea, Marekani huwa gharama za daktari, wauguzi na hospitali zinalipwa tofauti. Pia, Doreen baada ya kutakiwa kufanyiwa matibabu ya juu zaidi kwenye Kituo cha Madona, Nebraska kinachoheshimika zaidi duniani gharama zake ni Dola 50,000 (Sh100 milioni) kuingia tu,” alisema.
Nyalandu alisema hata gharama za ndege ya Samaritan Purse inakadiriwa kufikia Dola 300,000 za Marekani (Sh600 milioni) kwa safari ya kutoka Marekani hadi Kia na kurudi, hali inayoonyesha kama ingekuwa kulipia gharama ingekuwa changamoto.
Wanafunzi hao waliondoka nchini Mei 14 kwa ajili ya matibabu kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Samaritan Purse linaloongozwa na Mchungaji Franklin Graham wa Marekani, ukiwa ni msaada wa taasisi yake baada ya kuombwa kufanya hivyo.
Kuhusu maendeleo ya afya zao, Nyalandu alisema wanaendelea vyema kutokana na kuwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa kwa miezi mitatu na wamejiridhisha kuwa wamepona.
Aliongeza kuwa itafanyika hafla fupi ya mapokezi Jumamosi (kesho) katika Shule ya Lucky Vincent na baadaye watakabidhiwa vifaatiba katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Akizungumzia ujio wa wanafunzi hao, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema ni mashujaa kwani Mungu ameokoa maisha yao.
Lazaro alisema ataungana na wakazi wa Arusha kuwapokea, lakini akaeleza kwa niaba ya Jiji la Arusha kuwa wanampongeza Nyalandu kwa kufanikisha matibabu ya watoto hao.
Alisema kama siyo jitihada binafsi za Nyalandu, wanafunzi hao tayari wangekuwa na vilema vya maisha au wangepoteza maisha.
“Tunampongeza sana Nyalandu kwa uzalendo wake na huu ndiyo utu na ubinadamu, sisi viongozi wetu wamejikita katika masuala ya kisiasa na kukomoana, lakini Nyalandu ameonyesha aina ya uongozi ambao hautasahaulika,” alisema Lazaro.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, walieleza kuwa wanajisikia furaha kurejea kwa wenzao na kutaka uongozi wa shule kutenga siku maalumu ya kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia.
“Tunashukuru wenzetu wamerudi salama, tutashirikiana nao tena waendelee na masomo, tuliwa-miss sana,” alisema Neema Alfred.
Mwanafunzi mwingine, Lucas Laizer alisisitiza uongozi wa shule hiyo kutenga siku maalumu kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia, kwa kuwa tukio hilo halitasahaulika kwenye historia ya shule yao.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Efraim Jackson alisema hatima ya wanafunzi hao kufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba unaoanza Septemba 6, itajulikana baada ya kupata mwongozo kutoka serikalini hasa kutokana na kutokuwapo darasani kwa muda.
“Siwezi kujibu moja kwa moja kama wana sifa za kufanya mitihani yao ya mwisho au la! Kwa sababu suala hili litategemea vyombo vingine lakini ngoja tuwapokee kwanza,” alisema.
Tags