Mbunge wa CCM Ashikiliwa na Polisi
0
August 11, 2017
Singida. Jeshi la polisi mkoani Singida linamshikilia Mbunge Manyoni(CCM), Daniel Mtuka (51) kwa tuhuma ya kumgonga kwa gari mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Sukamahela, Salome Paschal (10) na kusababisha kifo chake papo hapo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, debora Magilingimba alisema tukio hilo limetokea jana katika Kijiji cha Sukamahela tarafa ya Kilimatinde Wilaya ya Manyoni.
Alisema siku ya tukio mbunge huyo akitokea Dodoma mjini akiwa njiani kurundi jimboni kwake akiendekesha gari lake aina ya Toyota Prado alimgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa akijaribu kuvuka kutoka upande wa kulia kwenda kushoto mwa barabara.
Kamanda huyo alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva Mtuka, kushindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Mtuhumiwa mbunge Mtuka anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano na baada ya mahojiano, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa uchunguzi wa daktari na baada ya hapo, utakabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi,”alisema.
Katika hatua nyingine, Kamanda Debora alisema watu wawili akiwemo Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ngara mkoani Kigoma, Alfred Kafuku wamefariki dunia papo hapo, baada gari walilokuwa wakisafiria kugonga lori aina ya DAF kwa nyuma.
Amewataja waliofariki kuwa ni dereva wa gari raia wa Congo ambaye jina lake halikuweza kupatikana na wala kitambulisho chake.
Tags