Mkuu Wa Mkoa Mjini Magharibi Atoa Taarifa Kuhusu Sikukuu Ya Eid El Hajj Kesho

Mkuu Wa Mkoa Mjini Magharibi Atoa Taarifa Kuhusu Sikukuu Ya Eid El Hajj Kesho
Ndugu wananchi wakaazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wasikilizaji na watazamaji.
ASSALAMU ALAYKUM,

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutujaalia neema ya uhai, uzima, amani na utulivu katika Mkoa wetu wa mjini Magharibi.

Ndugu wananchi kama mjuavyo kuwa siku ya Ijumaa ya tarehe 1/9/2017 tutasherehekea sikukuu ya Eid El Hajj ambapo waislamu wote duniani wataungana na mahujaji waliopo Makka Saudi Arabia baada ya kukamilisha nguzo ya tano ya kiislam kwa kutekeleza ibada ya Hijja ambayo ni lazima kwa mwenye uwezo.

Ndugu wananchi pamoja na wakaazi wote wa Mkoa wa Mjini Magharibi  napenda nichukuwe fursa hii  kutoa taarifa inayolenga kuwanasihi na kukumbushana mambo muhimu ya kuzingatiwa  katika kipindi chote cha skukuu na  baada ya skukuu ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi ili kuendeleza na kudumisha amani iliyopo.

Kwa mwaka huu wa 2017 swala ya eid itafanyika Wilaya ya Magharibi B katika kiwanja cha Dimani na Baraza la Eid litafanyika Bweleo katika eneo la mapumziko la wananchi karibu na nyumba mpya za Fumba.

Jambo la msingi nawaomba wananchi wote tusherehekee sikukuu hii katika hali ya Amani na utulivu kama ilivyo desturi yetu.

Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa katika kipindi chote cha sikukuu.

Vilevile, vitendo vya ukiukwaji wa sheria za usalama wa barabarani vinavyofanywa na baadhi ya madereva wazembe  vitadhibitiwa na kutakuwa na operesheni maalum ya ukaguzi wa vyombo vyote vya moto yakiwemo magari na vyombo vya magurudumu mawili.

Tahadhari ya kudhibiti mwendo itachukuliwa kwa kuwekwa vizuizi katika maeneo mbali mbali ya barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kugharimu uhai wa wananchi wetu.

Hivyo, napenda nitoe wito kwa madereva wa vyombo vya moto hasa madereva wa daladala na wamiliki wa vyombo binafsi vya usafiri kuchukua tahadhari ya hali ya juu hususan wakati wa jioni    wanapowapeleka watoto  katika viwanja vya skukuu. Aidha, tunawaomba watumiaji wa vyombo hivyo kuhakikisha kuwa vyombo vyao vimekaguliwa na mamlaka husika za ukaguzi na kupatiwa ruhusa ya kukubalika kwa vyombo hivyo kutumika barabarani kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni ya njia(road licence) pamoja na bima (insurance). Hivyo, kwa taarifa hii, Mkoa unaagiza kuwa wale wote ambao vyombo vyao havijapasishwa na mamlaka husika, wasiviingize vyombo hivyo barabarani kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi na kusababisha ajali zinazoweza kuepukika.

Pia, naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha madereva na utingo wa daladala kutopandisha  viwango vya nauli nyakati za usiku kwa njia zote za  Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kuhusu Viwanja vya sikukuu, vitakavyotumika ni  (29) na vitaanza shughuli zake wakati wa alasiri na muda wa kufunga utatofautiana kutokana na mazingira ya viwanja hivyo kama ifuatavyo.

Wilaya ya Mjini
Viwanja vya skukuu  ambavyo vitatumika ni Mnazimmoja, Viwanja vya Demokrasia (Kibandamaiti), Kariakoo, Mnara wa kumbukumbu (mapinduzi square), Jamhuri Garden, Mnazi mmoja na Forodhani park mbapo viwanja hivi vyote vitaanza shughuli zake kuanzia saa 10:00 jioni na kufungwa saa 4:00 usiku.

Wilaya ya Magharibi “A”:
Viwanja vitakavyotumika ni kiwanja cha Dole, Kihinani Melinane, skuli ya Mbuzini, Jazira Kigorofani, Jazira, Skuli ya maandalizi ya Mfenesini na Zanzibar Park (Viwanja hivi vitaanza saa 10:00 na kumaliza saa 4:00 usiku.

Viwanja vyengine ni Skuli ya Maandalizi Mfenesini, Garagara, Kijichi kwagube, Stella Darajabovu, Kihinani Zantel, Skuli ya Regezamwendo na Mwakaje (Viwanja hivi vitaanza saa 10:00 na kumaliza saa 1:00 usiku)

Wilaya ya Magharibi “B”
Viwanja vitakavyotumika ni : Skuli ya Sekondari Biashara, Viwanja vya Magereza, Maungani, Kwa bamgeni Pangawe, Kiembesamaki kwa Abdalla Rashid, Kinuni, na Fumba (Viwanja hivi vitaanza saa 10:00 jioni na kumaliza saa 4:00 usiku)

Viwanja vyengine ni : Nyarugusu, Magirisi na Skuli ya Private Kwarara Progressive ambavyo vitaanza saa 10:00 jioni na kumaliza saa 1:00 usiku)

Viwanja ambavyo havikutajwa havitaruhusiwa kufanyika skukuu.
Aidha, Kwa upande wa Wilaya ya Magharibi “B” kutakuwa na kiwanja kipya cha skukuu katika eneo la kupumzikia la fukwe ya bahari ya fumba eneo linalojengwa nyumba za  kisasa za makaazi fumba.
Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Idara ya Usafiri na leseni imeandaa usafiri maalum wa daladala ya rout ya Fumba kwa lengo la kuwarahisishia wananchi kufika na kurudi katika kiwanja kipya cha skuu kiliopo fumba kwa urahisi.

Ndugu wananchi, nachukua nafasi hii kuendelea kukumbusha kuwa suala la upigwaji muziki ni marufuku katika viwanja vyote vya  sikukuu, wakati ambapo katika vilabu na kumbi za starehe  wataendelea kufuata utaratibu wa muda uliowekwa  na Serikali ambapo watatakiwa kupiga muziki kuanzia saa 2:30 usiku na kumaliza sa 6:00 usiku. isipokuwa holi la bwawani na ukumbi w ngalawa ambayo mwisho ni saa 8 usiku.

Serikali ya Mkoa itaendelea kufuatilia utekelezwaji wa maagizo haya na kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria wale wote watakaokiuka taratibu hizi.

Ndugu wananchi kuhusu uuzwaji wa vyakula katika viwanja vya skukuu nawaomba sana wafanya biashara wote kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali kupitia  Mabaraza ya manispaa kwa kushirikiana na Wizara ya afya kwa kupata vibali vya kufanya biashara pamoja na kuimarisha usafi wakati wote ili kuepusha athari zinazoweza kutokea ikiwemo mripuko wa maradhi ya kipindupindu.

Ndugu wananchi Napenda nitoe nasaha zangu kwenu wazazi na walezi kutowaacha watoto wadogo kutembea peke yao katika barabara na viwanja vya sikukuu ili kupunguza tatizo la kupotea kwa watoto katika kipindi hicho.

Kabla ya kumalizia taarifa yangu hii, ninawakumbusha wananchi wote kufuata maagizo ya Serikali kwa kutii sharia bila ya shuruti.

Ndugu wananchi kwa kuwa hivi sasa nakaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja naomba nitumie fursa hii kuwanasihi wananchi wezangu wa Mkoa huo kuendelea kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha sikuu na siku zijazo.

Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuendelea kuwa na Amani na utulivu katika Mkoa wetu wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini unguja na Zanzibar kwa ujumla

Tunamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie ndugu zetu waliokwenda kutekeleza ibada ya hijja awakubalie hijja zao na warejee nyumbani wakiwa salama.

Na kwale ambao  bado hawaja jaaliwa kwenda kutekeleza ibada hiyo tumuombe Mwenyezi Mungu kwa Baraka zake atushushie neema hiyo ili nasi tuweze kutekeleza nguzo hiyo ya kiislam.
Eid Mubarak.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad