MWANAMUZIKI wa miondoko maarufu kwa jina la Tanzania, Kenya na Uganda (Takeu), ambaye alijizolea umaarufu miaka ya 2000 na baadaye kupotea kidogo kutokana na sababu za hapa na pale, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ amesema kuwa anaamini kuna baadhi ya Watanzania wenzake hawampendi.
Mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa amerejea upya katika gemu, amefunguka mambo mengi katika makala haya:
Showbiz: Mashabiki Bongo walikumisi kwa muda mrefu wangependa kujua ulikuwa wapi na unafanya nini kwa sasa?
Mr Nice: Maisha yangu kwa sasa yapo Kenya, huko nina zaidi ya miaka mitatu nikifanya muziki wangu, nimeamua kuhamishia makazi huko kwa sababu kule wenzetu mambo ya burudani wako mbali sana hivyo kazi zinapatikana kwa wingi tofauti na Bongo.
Showbiz: Vipi kuhusu mazingira ya huko hayakukupa shida? Mr Nice: Hapana halafu unajua maisha yangu ya muziki yamekuwa ya kwenda hapa na pale nchi mbalimbali hivyo hiyo haikunisumbua.
Showbiz: Unazungumziaje habari zilizokuwa zikizagaa kuhusu kifo chako?
Mr Nice: Ni chuki tu za baadhi ya Watanzania wenzangu na ninashindwa kuelewa kwa nini wananichukia kiasi hiki wakati nchi nyingine wananiona lulu? Kwa nini wananifanyia hivyo wakati Kenya naishi kama mfalme maana hata nikiambiwa nije kufanya shoo Tanzania, najifikiria mara mbili mbili kwa sababu naona watu wangu wamenitenga.
Showbiz: Kuna siku ulikuwa ukiimba wimbo wako wa Mama huku ukibubujikwa na machozi na kusema unaumia watu wanasema una ugonjwa wa Ukimwi, unazungumziaje hilo?
Mr Nice: Ni kweli watu walinipakazia hivyo na wimbo ule wa Mama unaniliza kwa sababu najua mama yangu angekuwepo angewakemea waache kuzungumza maneno hayo maana mastaa wenye mama zao wakisakamwa tu, mama zao wanaibuka kukanusha.
Showbiz: Kwa nini unasema baadhi ya Watanzania wanakuchukia? Mr Nice: Kwa sababu wamekuwa ni watu wa kunidharau, kunidhihaki kwa sababu heshima ambayo ningeipata hapa nyumbani naenda kuipata nchi nyingine.
Showbiz: Mashabiki wako wangependa kufahamu huko Kenya upo na familia yako?
Mr Nice: Kenya, nafanya kazi tu, familia yangu yote ipo Tanzania, lakini sijaoa na wala sitegemei kufanya hivyo kwa sababu tayari nina watoto wawili ambao nataka kuwalea bila karaha ya mama wa kambo.
Showbiz: Najua muigizaji Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’ huko nyuma alikuwa ni mpenzi wako vipi unazungumziaje kuhusu matatizo yaliompata?
Mr Nice: Namuombea ila kwa upande wa Watanzania, waache kushabikia mtu anapopatwa na janga na kuanguka. Wamuombee na waache manenomaneno.
Showbiz: Ni faida gani umeipata mpaka sasa kutokana na muziki?
Mr Nice: Nyingi sana, kwanza nina mijengo ya maana minne, nina usafiri wangu na nina mashamba kutokana na muziki huohuo na miradi yangu mingine mingi.