IDARA ya Uhamiaji nchini imewataka wananchi kutambua kuwa paspoti siyo kitambulisho ndani ya nchi na kwamba kisitumike kwa matumizi hayo kwa sababu siyo utaratibu uliopangwa kisheria ndani ya mipaka ya nchi.
Pia amesema kuwa ikibainika kuwa mtu amepoteza paspoti hiyo kizembe hatopewa nyingine. Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Uhamiaji- Pasi na Uraia, Gerald Kihinga wakati alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili, na kuwaomba wananchi kutambua kuwa paspoti zinazotolewa zinapaswa kutunzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa la kusafiria nje ya nchi.
Kihinga alisema kumekuwa na maombi ya kutengenezewa paspoti baada ya kupotezwa, lakini wengi wamekuwa wakitoa sababu ambazo zinatilia shaka umakini wa mtu kwenye utunzaji wake. “Naomba mfahamu kuwa paspoti pia zinazotolewa siyo vitambulisho ndani ya nchi hivyo visitumike kama vitambulisho na tena si vizuri kutembea nayo kila mahali kama huna safari ya nje ya nchi.
Paspoti au hati ya kusafiria zinatumika kama kitambulisho pale unapokuwa nje ya nchi, lakini matumizi yake rasmi ni ya kukusaidia kuingia na kutoka nchini,” alisema. Alisisitiza kuwa kitambulisho rasmi cha Mtanzania anachotakiwa kutembea nacho ni kile kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Aidha, kamishna huyo pia ametaka wananchi raia wa Tanzania kutambua kuwa wanaweza kupata paspoti wakiwa popote Tanzania na kwa muda mfupi.