Naandika kama mnunuzi au muuzaji wa aina hio ya magari, kwahio siegemei upande wowote na ninachokiandika hapa sio sheria naweza kuwa sahihi au nisiwe sahihi ila ni imani yangu lipo litakalosaidia baadhi ya watu.
Njia muhimu za kufuata ili kupata gari unalotaka ni kama ifuatavyo:
1. Fanya utafiti mdogo juu ya gari unalolitaka: Uliza ujue gari unalolitaka linauzwa kiasi gani[makadirio]. Ukiweza kujua bei ya showroom au ukiagiza mwenyewe Japan halafu linganisha na bei utakayopewa hapa. Hili ni muhimu kwa sababu nimeshuhudia watu wananunua magari yaliyotumika Tanzania kwa bei ambayo ukiagiza mwenyewe unalipata kutoka japan au ukiongeza kidogo tu unapata la showroom.
2. Usiwe na haraka: Usiwe na haraka kabisa kwenye kutafuta gari. Utaletewa kila aina ya gari na usipokuwa makini utanunua gari bovu. Angalia taratibu angalau magari matano tofauti kwenye chaguo lako ndipo uamue, madalali watakusumbua ili mradi tu wapate cha juu.
3. Epuka madalali: Kama unaweza epuka madalali. Tafuta gari kwa kuuliza watu ulio karibu nao, ndugu jamaa na marafiki au unaofanya nao kazi au biashara. Hii ni nzuri chochote kikitokea una pa kuanzia. Madalali wengi hawajali maslahi yako wala ya muuzaji cha muhimu kwao ni cha juu tu. Gari la 4m dalali atakuuzia 5-6m.
4. Tafuta Fundi: Ukilipenda gari lolote tafuta fundi akusaidie kulikagua, hata kama una ujuzi(idea) na magari kuna vitu hutaviona ila fundi atakusaidia. Kuwa makini kuna mafundi huwa wanabonyezwa wakufiche hitilafu halafu baadae wanarudi kupewa chao ukishauziwa kanyaboya.
5. Epuka gari lililopigwa rangi: Epuka gari iliopigwa rangi siku chache kabla ya kuwekwa sokoni, wazoefu wanajua gari za aina hio ndio umuhimu wa fundi unapokuja. Gari inaweza kuwa imegongwa hivyo imenyooshwa na wanakuzuga kwa rangi inayong'aa. Siku hizi rangi hata 200,000 unapiga gari nzima ila ukinunua hilo baada ya mwezi rangi inababuka yote.
6. Epuka gari lililooshwa engine: Ukikagua gari ukiona limeoshwa engine ogopa sana. Mara nyingi magari yanaoshwa engine kuficha 'leakage', yaani oil na vitu vingine vinavyovuja kutoka sehemu mbalimbali za engine.
7. Jaribu gari wewe mwenyewe: Ni muhimu kuendesha na kuijaribu gari wewe mwenyewe hata ukienda na fundi. Ipitishe njia mbovu usikie jinsi ilivyo chini, chochote kinachogonga kuwa makini, usisikilize ukiambiwa ni tatizo dogo, kwanini hakurekebisha. Ingawa yapo matatizo madogomadogo ila kuwa makini.
8. Usiangalie plate Namba: Usibabaishwe na namba, eti hii C, D etc. Kuna gari namba A ziko vizuri kuliko namba C. Muhimu ni hali ya gari husika kwa muda huo.
9. Nenda TRA kujiridhisha: Ni muhimu kujua ukweli na status ya gari na mwenye gari. Jiridhishe anaekuuzia ndio mwenye gari. Akuonyeshe nyaraka zote halisi hata za kodi aliolipia.
10. Mwisho kabisa ukilipenda gari fanyeni makabidhiano kwa kuandikishana kwa mwanasheria. Ukiweza lipia benki na ubaki na risiti kama ushahidi wa malipo kupitia akaunti yake. Epuka kubeba cash kumpelekea muuzaji mahali alipo.
Haya machache naamini yanaweza kuwa msaada kwa watu wanaonunua magari yaliyotumika nchini,wengine mnaweza kuongezea mawili matatu na kurekebisha nilipokosea.