Mwanafunzi Afungwa Jela Miaka 20, Akutwa Akiwaonesha Wanafunzi Picha za Ngono Kupitia Simu yake ya Mkononi

Mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Tawi la Tabora Marick Mbega amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kuwadhalilisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Isike mkoani hapa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Emmanuel Ngigwana alitoa adhabu hiyo juzi baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka wakiwamo wanafunzi waliodhalilishwa.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Upendo Malulu uliieleza Mahakama kuwa Mbega alitenda makosa hayo Aprili 4 mwaka huu, kinyume na kifungu namba 138 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya 2002.

Wakili Malulu alidai siku hiyo katika eneo la Shule ya Msingi Isike katika Manispaa ya Tabora, mshtakiwa alikutwa akiwaonesha wanafunzi picha za ngono kupitia simu yake ya mkononi.

Alisema mbali na Mbega kuwashawishi wanafunzi hao wamshike sehemu za siri, pia alikuwa akiwachezea.

Wakili Malulu alisema baada ya kufanya upekuzi katika simu ya mshtakiwa, ilikutwa ikiwa na picha 197 za ngono na video 40 zikiwamo za watoto, watu wazima na wanyama.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Ngigwana alisema mtu anayeonyesha sehemu zake za siri, kuchezea za watoto, kuonyesha picha za ngono au filamu za ngono anafanya udhalilishaji na ni kinyume cha sheria.

Alisema mtoto hana uamuzi kisheria, hivyo hawezi kuchukuliwa kwamba alikubali matendo hayo.

Hakimu Ngigwana alisema Mahakama imeona mashtaka ni mtu mzima tena Mwanafunzi wa Chuo cha Umma aliyedhaniwa kuwa na maadili kwa jamii, mstaarabu, mwenye kujali, kulinda na kutetea maslahi ya watoto, lakini alitenda kosa hilo, hivyo anastahili adhabu.

Pia, alisema mshtakiwa alipaswa kuhakikisha mtoto anakuwa vizuri kiakili, kimwili, kiroho na kisaikolojia badala yake amekwenda kinyume.

Alisema ili iwe fundisho kwake na onya kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo, atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka kumi jela kwa kila kosa.

Chanzo: Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad