Ndugai Kukinukisha Ripoti Mpya ‘Makinikia’ ya Almasi

Ndugai Kukinukisha Ripoti Mpya ‘Makinikia’ ya Almasi
WAKATI Spika wa Bunge, Job Ndugai akiahidi kuwekwa wazi wiki ijayo kwa ripoti ya kamati mbili zilizochunguza uchimbaji wa madini ya almasi na tanzanite nchini, imebainika kuwa yale yaliyomo kwenye ripoti kuhusu vito hivyo yataibua kishindo cha aina yake.

Spika Ndugai aliunda kamati hizo mwezi uliopita na kuzipa siku 30 kuanzia Julai 10, 2017 ziwe zimekamilisha kazi zake. Alichukua uamuzi huo katikati ya mjadala mzito kuhusiana na kile kilichoibuliwa na ripoti za kamati mbili za rais zilizochunguza usafirishaji nje ya nchi wa mchanga wa madini (makinikia).

Kubwa ilibainika katika ripoti za kamati hizo zilizoongozwa na Prof. Abdulkarim Mruma na nyingine ya Prof. Nehemiah Osoro, ikiwamo kuwapo kwa tofauti kubwa ya kile kilichokuwa kikiripotiwa na kiwango halisi cha madini yaliyokutwa kwenye makontena 277 yaliyoshikiliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliipelekea Kampuni ya Mgodi ya Barrick madai ya kodi iliyolikmbikizwa tangu mwaka 2000 na adhabu ya jumla ya dola za Marekani bilioni 190 (zaidi ya Sh. trilioni 420),

Wakati akiunda kamati hizo na kumteua Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu kuwa mwenyekiti, Ndugai alizipa jukumu la kutoa ripoti ya kushauri juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini hayo nchini.

Juzi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Spika Ndugai alisema angeenda Dodoma jana (Ijumaa) na kukutana na wajumbe wa kamati hizo ili kupata mrejesho wa uchunguzi.

"Ni kweli niliunda kamati mbili za Bunge  zenye wajumbe 11 ili kufuatilia uuzwaji wa madini nje  ya nchi… niliipa siku 30 na wiki ijayo nitatoa mrejesho," alisema Ndugai.

Aidha, maelezo hayo ya Spika yalihitimisha taarifa mbalimbali zilizodai kuwa kamati alizounda zimeshindwa kukamilisha majukumu yake kwa wakati kutokana na uhaba wa fedha. Kimahesabu, kamati hizo zilizokabidhiwa majukumu Julai 10, zilitarajiwa kukamilisha kazi zake walau kufikia Agosti 10, 2017.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa licha ya changamoto mbalimbali zilizopo, kazi za kamati zimeenda vizuri na kwamba ripoti inatarajiwa kuibua kishindo kingine kisichotofautiana sana na ilivyokuwa katika ripoti za kamati mbili za makinikia ya dhahabu zilizoundwa na Rais John Magufuli.

“Unajua nchi hii imekuwa hainufaiki ipasavyo kupitia rasilimali zake kutokana na utata wa mikataba iliyokuwa ikisaniwa na wale waliopewa dhamana,” chanzo kiliiambia Nipashe na kuongeza:

“Hizi kamati za Spika zimefanya kazi nzuri sana…kutakuwa na mengi yatakayotoa nafasi kwa taifa kunufaika na rasilimali hizi (almasi na tanzanite).

“Ni suala tu la kusubiri ili wakati ukiwadia ripoti zake ziwekwe wazi ili Watanzania wajue kila kinachofanyika.”

CHANZO KAMATI ALMASI, TANZANITE
Juni 2, mwaka huu, Spika pia aliunda kamati yenye wajumbe tisa kwa ajili ya kuchunguza uchimbaji na biashara ya Tanzanite ambayo vilevile ilitakiwa kufanya kazi hiyo ndani ya siku 30 mara baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti.

Akizungumza kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti Julai 5, mwaka huu, Spika alisema ameunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika Na.3 wa mwaka huu.

“Kamati hii itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini,” alisema.

Mbali na Zungu, wajumbe wengine wa kamati hiyo ni pamoja na Wabunge wa Viti Maalum, Dk. Immaculate Semesi (Chadema), Shally Raymond na Restituta Mbogo (wote CCM), Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM) na Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF).

Wengine ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) na Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM).
“Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa siku 30 kuanzia Julai 10, na Kituo Kikuu cha kazi kitakuwa katika Ofisi ya Bunge hapa Dodoma,” alisema Spika.

Aidha, hadidu za rejea za kamati hiyo zilikuwa ni pamoja na kuchambua taarifa za tume na kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na serikali kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini na kuona mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na serikali.

Kadhalika, wakati anatangaza kuunda kamati ya kuchunguza tanzanite, Spika Ndugai alizitaja hadidu za rejea za kamati hiyo kuwa ni pamoja na kuchambua mkataba kati ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Kampuni ya Tanzania One Mining kwa lengo la kubainisha manufaa na hasara ambayo nchi inapata kutokana na mkataba huo.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/16 zilizokabidhiwa kwa Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27 kisha kuwasilishwa bungeni Aprili 13, mwaka huu, zinabainisha upungufu mkubwa katika sekta ya madini nchini hususani dhahabu, almasi na Tanzanite.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Huku ndiko kunavyotakiwa katika kumsaidia Mh.Raisi.(JPM)
    Kila mmoja kwa sehemu yake anawajibika. Pamoja sana Ndungai

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad