NEC Yakosolewa na Wasomi Wataka Iige Mfumo wa Uchaguzi wa Kenya

   
NEC Yakosolewa na Wasomi Wataka Iige Mfumo wa Uchaguzi wa Kenya
 Baadhi ya wasomi wameikosoa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakiitaka kujifunza mfumo wa uchaguzi wa Kenya ambayo imefanya uchaguzi mkuu hivi karibuni.

Katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini Kenya, ukisimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC), Rais wa ncghi hiyo Uhuru Kenya (Jubilee) alimshinda mpinzani wake wa karibu Raila Odinga anayeongoza muungano wa Nasa kwa takriban asilimia 10 ya kura zote.

Hata hivyo Odinga amepinga matokeo hayo akilalamikia utendaji mbovu wa IEBC uliomsababisha yeye na chama chake kushindwa.

Licha ya kasoro hizo, baadhi ya wasomi wamesema mfumo wa uchagizi wa Kenya ni bora na wa kupigiwa mfano na nchi za Afrika.

Wakijadili suala hilo juzi usiku katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na televisheni ya ITV, wasomi hao walishauri kuwepo na mabadiliko ya Katiba ili kuboresha mfumo huo ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk Bernard Achiula alisema kukosekana kwa taasisi madhubuti za uchaguzi kumechangia manung’uniko kwa nchi nyingi za Afrika, huku pia akihoji muundo wa NEC.

“Narudia tena kwenye tume ya uchaguzi, hivi hapa Tanzania inaundwaje kwa mfano? Inaundwa na vyama vyote? Kwa Zanzibar sawa, lakini hapa (Bara) hakuna. Labda na sisi Tanzania Bara tujifunze kwa Kenya, kuvichukua vyama vya upinzani pengine italeta kidogho kuaminika,” alisema Dk Achiula.

Aliongeza kuwa kinachowafanya watu wakatae matokeo ni mfumo dhaifu wa taasisi za uchaguzi.

“Kwanza tujifunze kwenye maandalizi, lazima tuwasifu walijiandaa vizuri. Kampeni zilikuwa shirikishi, kulikuwa na elimu, masheikh walitumia muda wao, makanisa, watu walitumia sana social media, kwa kweli kampeni zilikuwa huru,” alisema Dk Achiula.

Sasa matatizo yanatokea kwenye hiyo hatua ya mwisho. Hatuwezi kusema kila kitu kilikuwa sawa.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Abdulkarim Atiki alishauri kuwepo kwa mfumo shirikishi katika tume ya Taifa ya uchaguzi uili iaminike.

“Tafsiri yangu ni kwamba usimamizi ni lazima uwe shirikishi zaidi. Kwanza tume inaundwa na nani? Unajua tume nyingi zinaundwa na ‘individuals’ tu?  Hili dude la tume ya uchaguzi linatakiwa liwe na uwakilishi wa kitaasisi kulikuwa kuwa la mtu mmoja mmoja,” alisema Atiki na kuongeza:

“Ukiniuliza mimi kwa maoni yangu, nitasema lazima kuwe na ‘representation’ (uwakilishi) ya wafanyakazi, intellectual community (wasomi), viongozi wa dini, hatuwezi kuepuka, matabaka yapo, hata Mwalimu (Nyerere) alisema haya matabaka yapo.”

Akifafanua zaidi, Atiki alishauri ushirikishwaji zaidi hata katika muundo wa Serikali kuliko mfumo wa sasa wa mshindi kuchukua vyote.

“Wajerumani wamemaliza matatizo kama hayo, kule Bavaria, kuna Westfalia, wametengeneza uchaguzi wao kiasi kwamba haiwezekani chama kimoja kikaunda Serikali. Kunakuwa na ‘coalition’, hiyo inasaidia kugawana keki ya Taifa,” alisema Atiki.

Atiki alishauri kurejewa kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ili kuweka mfumo imara wa uchaguzi huku akishauri pia kuwekwa kwa kipengele cha kupinga matokeo ya Rais mahakamani.

“Kwa wenzetu Kenya, pamoja na matatizo wanayoyapata, marekebisho ya Katiba yamewasaidia sana hali hii ya kwenda mahakamani,” alisema na kuongeza:

“Hili ni suala la kwenda mahakamani ni la muhimu sana. Nawapongeza sana Jubilee lakini zuio hili linanizuia, kuna siku 14, chochote kinaweza kutokea. Kwa hiyo wale wanaoipongeza Kenyatta wanafanya haraka, tusubiri kwanza siku 14.”

Aliongeza: “Kama ingekuwa ya zamani nadhani balaa lingekuwa kubwa zaidi. Kwa hiyo tujaribu na sisi. Ukimwona mwenzako ananyolewa basin a wewe tia maji ukinyolewa kavukavu utaumia

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Profesa Mbwiliza Joseph alipinga uwakilishi wa vyama kwenye tume za uchaguzi akisema ndiyo inachangia upendeleo katika matokeo, badala yake alishauri kuwe na uwakilishi wa taasisi nyinginezo katika kuteua uongozi wa tume.

“Sisi hapa kwa mfano tunaangalia ‘profession’ (taaluma) kwamba hawa ni wasomi, lakini ndani ya wasomi wapo kina Profesa Mbwiliza makada wa CCM,” alisema na kuongeza:

“Sasa m,nakuja mnaniangalia kwenye kundui la wasomi mnasema Profesa Mbwiliza mzee sana yule tena amekaa karibu miaka ya 80 anafundisha tu, kwa hiyo tumpe heshima yake akawe mwenyekiti wa tume.

“Nitapata matatizo aliyoyapata Jecha (Salum Jecha- Mwenyekiti ZEC) kwa sababu nitakaposimama kutangaza kushindwa kwa CCM nitapata kigugumizi na kwamba nimekwenda pale kwa tiketi hiyo, itakuwa ngumu,” alisema Profesa Mbwiliza.

Alishauri kuwepo na uangalizi wa karibu kwa viongozi wa tume ili kuepusha makada wa vyama watakaopendelea vyama vyao.

“Huyu ni Jaji ambaye tunasema asiwe upande wa chama, huyu ni Jenerali wa Jeshi awe huru. Kumbe hamkujua, huyu ni CUF wa kutupa. Sasa ni lazima tuwe waangalifu,” alisema.

Naye Dk Bashiru Ali ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema miongoni mwa mambo ya kujifunza kwa uchaguzi wa Kenya ni kurughusu wagombea huru, wafungwa na wananchi waishio nje ya nchi (diaspora) kupiga kura.

“Kwa wenzetu Kenya wamefikia hatua nzuri, siyo tu kuwaruhusu wafungwa (kupiga kura) bali hata kwa watu wanaokaa nje ya nchi na kwa wagombea binafsi. Mtu siyo kwamba ana haki ya kujiandikisha na kupiga kura bali opia ana haki ya kugombea bila kulazimishwa kuwa kwenye chama,” alisema na kuongeza:

“Tumekuwa na mjadala huo kwa muda mrefu na Mwalimu katika mambo ambayo tunamwenzi, alikuwa na msimamo kwamba huyo mgombea huru hawezi kufika mbali. Wagombea wenye vyama ndiyo wanakuwa na nguvu kwa sababu anakuwa na program, wanakuwa na mshikamano na rasilimali za chama.”

Alipoulizwa kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima alisema tume hiyo iko huru kwa mujibu wa Katiba.

“Soma vema Katiba JMT na sheria ya Uchaguzi ibara ya 74(7), (11) na 12 utaona uhuru wa Tume, ipo ‘very clear’ (wazi sana),” alisema Kailima




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad