Akizungumza na gazeti hili jana, Niyonzima alisema kiwango walichoonyesha katika mechi dhidi ya Rayon ni sehemu ndogo ya "ufundi" walionao wachezaji wa timu hiyo ambao msimu ujao wamejipanga kuipa klabu yao mataji.
Kiungo huyo aliyetua Simba hivi karibuni kwa kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, alisema kila mchezaji aliyesajiliwa Simba anafahamu kiu ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ambao wamekosa ubingwa kwa miaka minne.
Niyonzima alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kujifua na kabla ligi haijaanza, watakuwa wameimarika zaidi kwa sababu wachezaji wote wamekamilika na wanafanya mazoezi ya pamoja.
"Tutakuwa wazuri zaidi ligi itakapoanza, tulionyesha kiasi kidogo tu cha uwezo wetu, naamini mashabiki wetu watafurahi zaidi," alisema kiungo huyo wa zamani wa APR.
Naye kipa Aishi Manula alisema kuwa kikosi chao kinaimarika zaidi kila siku zinavyoongezeka huku ushindani wa namba ukiongezeka.
"Kambi ilianza kwa makundi, baadhi tulikuwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars) na wengine mchakato wa usajili ulikuwa haujakamilika, sasa tuko pamoja na tunaahidi kuendelea kujituma," alisema kipa huyo aliyetua Msimbazi akitokea Azam FC.
Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema kuwa wako katika mazungumzo ya mwisho ya kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo inatarajiwa kufanyika kesho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.