Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) umeahirisha kikao cha kutoa tangazo kuhusu mweleko wa chama hicho kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga alikuwa ameahidi kwamba angetangaza ni hatua gani atachukua leo baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa Ijumaa, ambapo mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.
Ajenti mkuu wa Nasa Musali Mudavadi amesema sasa muungano huo unapanga kutoa tangazo keshi Jumatano.
"Tunasikitika kwamba mashauriano yanachukua muda mwingi kuliko ilivyotarajiwa na Nasa kwa hivyo hawataweza kuwahutubia Wakenya kama walivyotarajia leo."
Bw Mudavadi hata hivyo amesema mashauriano "yanaendelea na yanaendelea vyema".
Hapo jana, Bw Odinga alikuwa ametoa wito kwa wafuasi wake kususia kazi kabla ya kutoa tangazo kubwa leo.
Watu wengi hata hivyo walionekana kupuuza wito wa kususia kazi.
Baada ya kutokea kwa maandamano katika baadhi ya maeneo ambayo ni ngome ya upinzani mitaa ya Mathare na Kibera jijini Nairobi na mji wa Kisumu, hali ya utulivu ilianza kurejea Jumatatu.