RAIS Uhuru Kenyatta amekiri kuwa, kama kuna kitu kilichomkosesha raha katika awamu ya kwanza ya utawala wake, basi ni matukio ya kigaidi yaliyofanywa mara kwa mara ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al Shabaab.
Ukiondoa jambo hilo, amesema kitu kilichomfurahisha sana katika utawala wake ni kukamilika na kuzinduliwa kwa mradi wa reli ya kisasa kati ya Mombasa na Jiji la Nairobi. Aliyasema hayo siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya, alipokuwa akijibu maswali ya Wakenya kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook.
Akizungumzia jambo lililomfurahisha zaidi, hakusita kusema kuwa ni kukamilika na kuzindua reli ya kisasa `Standard Gauge Railway (SGR)’ naye kusafiri kwa treni kutoka Mombasa hadi Nairobi. Reli hiyo ya kisasa ilizinduliwa Mei mwaka huu na hivyo kuashiria ukuaji wa sekta ya usafirishaji nchini Kenya. Aidha, reli hiyo imesaidia kuimarisha usafiri wa kwenda na kutoka Mombasa.
Mbali ya kuwa ni usafiri wa uhakika, nauli ya treni pia ni nafuu huku ikisafiri kwa saa nne tu kati ya Nairobi na Mombasa, umbali wa kilometa 441, sawa na maili 271. Kuhusu kilichomsononesha akiwa madarakani, alisema ni mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Al Shabaab.
Kundi hilo, kwa nyakati tofauti limefanya mashambulizi huko Lamu na Kaskazini Mashariki mwa Kenya na kuua watu kadhaa. Na tukio la hivi karibuni huko eneo la Milihoi liliua watu watatu, huku Karibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Maryam El Maawy akipigwa risasi begani. Rais Kenyatta anatarajiwa kuapishwa wakati wowote baada ya kuwa ameshinda kwa mara nyingine uchaguzi mkuu, akimbwaga mshindani wake wa karibu, Raila Odinga.
Rais Kenyatta Anyoosha Mikono Kwa Al Shabaab...Akiri Kuwa Wanamnyima Raha...
0
August 21, 2017
Tags