Rapa Roma Mkatoliki amefunguka na kudai hana deni analodaiwa na mashabiki zake mpaka sasa ila anachojua yeye kuwa ndiyo alikuwa anawadai na ameshalipwa baada ya wao kupiga kelele za 'free Roma' kipindi alipotoweka.
Roma amebainisha hayo siku za hivi karibuni baada ya watu wengi kudai msanii huyo anadeni la kulilipa kwa wananchi kwa kuwa hajazungumza jambo lolote lililomsababisha yeye mpaka kutekwa na watu wasiyojulikana.
"Mimi ndiyo naweza kusema niliwakopesha washkaji deni maana ndani ya miaka 10 nimeimba nyimbo za kiharakati, changamoto pamoja kero za jamii vyote nawaimbia watu bila ya kulipwa chochote. Leo limenikuta la kunitokea wananchi basi wameungana kutokana na ngoma zangu wamepaza sauti zao, ukiniambia mimi nina deni ni kama wao wamenilipa kwa sababu mimi niliwakopesha kupitia ngoma zangu", alisema Roma.
Pamoja na hayo, Roma amesema hadhani kama chochote atakachokieleza kwa umma wataweza kuridhika kutokana na tukio lake jinsi lilivyokuwa.
"Sidhani kama kuna majibu sahihi ukamwambia mtu akaridhika kuhusiana uhalisia wa tukio lililonitokea mimi, sina cha kufanya zaidi kusema asante kwa kupaza sauti zenu mpaka kupatikana kwangu, maisha yaendelee, nipo poa, nipo strong, niombeeni tuendelee", alisisitiza Roma.
Video mpya ya Roma Mkatoliki 'Zimbabwe' aliyoiachia Agosti 10 mpaka sasa imeweza kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza kuwa 'trending' za video katika mtandao wa Youtube.