Tanzania Yapewa Onyo na Freemason




Tanzania Yapewa Onyo na  Freemason
Jumuiya hiyo, ambayo inatambuliwa na Jumuiya Kuu ya Freemasons nchini Uingereza (United Grand Lodge of England), ilitoa tahadhari yake rasmi jana, baada ya kuwapo kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwapo kwa upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kupitia matangazo yanayoelezea utaratibu wa kujiunga uanachama katika namna isiyokuwa sahihi.

Hivi karibuni, kumekuwa na matangazo mbalimbali katika maeneo ya miji, ikiwamo Dar es Salaam, yanayohamasisha watu kujiunga na jumuiya.

Vyanzo mbalimbali vimeiambia Nipashe kuwa hadi sasa, tayari baadhi ya watu wameshalizwa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na matumaini wanayopewa na matapeli wanaojinadi mitaani kuwa wanawaunganisha watu kuwa ‘memba’ wa Freemasons kwa kuwatoza fedha huku pia, wakiwapa matumaini hewa kuwa shida zao kiuchumi zitafikia mwisho na kuwa mabilionea wakubwa kupitia jumuiya hiyo.

Mbali na matangazo yanayotolewa kupitia mabango mbalimbali ya mitaa ya maeneo ya miji ikiwamo Dar es Salaam, hamasa za kuwataka Watanzania wajiunge uanachama wa Freemasons zimekuwa pia zikisambazwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii huku ahadi kubwa ikiwa ni kuwakwamua watu kiuchumi.

Hata hivyo, katika taarifa iliyosambazwa na Freemasons, ambayo ilitolewa kama tangazo jana, na kuidhinishwa na Dar es Salaam Masonic Trust, Watanzania wametakiwa kujiweka mbali na mtangazo yanayohusiana na hamasa ya kuwataka wajiunge kuwa wanachama wa Freemasons kwa sababu kinyume chake, watajiweka katika hatari ya kutapeliwa.

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa Freemasons haitahusika wala kuchukua dhamana kwa mtu au watu watakaotoa fedha kama malipo ya kujiunga na jumuiya hiyo.

“Jumuiya ya Freemasons inapenda kutoa taarifa na tahadhari kwa umma kuwa kumekuwako na matangazo ya aina mbalimbali yanayotolewa na watu wasio na uhusiano wowote na jumuiya hii.

“Kwa hivyo tunaufahamisha umma kuwa jumuiya ya Freemasons haihusiki wala haihusiani na mtu, watu au kikundi chochote kinachotangaza kwa lengo la kutafuta wanachama,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Freemasons.

POLISI WAFUNGUKA
Katika hatua nyingine, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lucas Mkondya, aliiambia Nipashe jana, kuwa hadi sasa hawajawahi kupokea malalamiko yanayohusiana na utapeli unaofanywa na watu wanaotumia jina la Jumuiya ya Freemasons nchini na kwamba, wako tayari kuchukua hatua stahili pindi jambo hilo likiwafikia.

Alisema ingawa upo uwezekano wa kuwapo kwa mabango ya aina hiyo mitaani, Jeshi la Polisi litakuwa na nafasi nzuri ya kufanyia kazi jambo hilo endapo litapata taarifa rasmi ambayo itatoka kwa wenye uhalali na jumuiya hiyo, ili liifanyie kazi.

“Pamoja na (Freemasons) kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari, bado hatuwezi kuanza kufanyia kazi taarifa ambazo hazijafikishwa kwetu.

Inawezekana ni kweli wanatumia jina la Freemasons, ili kujipatia fedha, kufanya utapeli… kazi yetu ni kupokea taarifa na kufanyia kazi,” alisema Mkondya.

UMAARUFU WA FREEMASONS
Freemasons wamejitwalia umaarufu nchini katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuwapo na taarifa zinazowahusisha wanachama wake na mafanikio makubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, hasa biashara.

Aidha, baadhi ya uvumi uliotanda kuhusiana na Freemasons ulionekana kuwa hauna ukweli kupitia ufafanuzi uliotolewa kwa nyakati mbalimbali na aliyekuwa mkuu wa jumuiya hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania na Shelisheli), Sir Andy Chande. Chande alifariki Aprili, mwaka huu.

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali, Freemasons husimamia msingi wa kuwa na agano miongoni mwa wanachama la kushirikiana kwa kila hali, ili kufikia malengo ya pamoja.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad