Jeshi la Polisi Mkoani Tabora limewafikisha katika Mahakama ya hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Nzega Mkoani humo watuhumiwa 32 wakiwemo viongozi wa kijiji na kata kwa mauaji ya wanawake watano wa kijiji cha Udoma kata Uchama.
Mwendesha Mashtaka wa jeshi la Polisi Wilaya ya Nzega Merito Ukongoji,mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya hiyo Sarafina Nsana, ameiambia Mahakama hiyo mnano tarehe 25 mwezi uliopita katika kijiji cha Undomo watuhumiwa hao waliwashambulia kwa kuwapiga na kuwachoma moto hadi kufa wanawake hao watano kwa tuhuma za ushirikina.
Merito amewataja wanawake hao waliouwa kwa kuchomwa moto ni pamoja na Sukuma Masali, Ester Kiswahili, Christina Said, Mwashi Mwanamila pamoja na kabuka Kagito, lakini watuhumiwa hao hawakupaswa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na Mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Baadhi ya Viongozi waliokamatwa kwa tuhumu hizo ni pamoja na Malewa Malonji, mtendaji wa kata ya Uchama, Karoli Masanja Diwani wa kata ya Uchama, pamoja na Doto Saraganda ambaye ni mtemi wa Sungusungu na kesi hiyo itatajwa tena tarehe 4 mwezi ujao na watuhumiwa wamerudishwa tena rumande.
Hata mauaji hayo yalitekelezwa Mwishoni mwa mwezi Julai huko katika kata ya Uchama Wilayani Nzega Mkoani Tabo kwa madai kuwa wanatekeleza imani za ushirikina.