Wafanyabiashara Wanaotoa huduma Uwanja wa Ndege (JNIA) Wapewa Mwezi Mmoja Kulipa Kodi na Prof. Mbalawa




Wafanyabiashara Wanaotoa huduma Uwanja wa Ndege (JNIA) Wapewa Mwezi Mmoja Kulipa Kodi na Prof. Mbalawa
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa Mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kulipa kodi ya Majengo kama mikataba yao inavyolekeza.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo leo wakati alipokutana na wafanyabiashara hao ili kujadili changamoto mbalimbali zilizopo na jinsi ya kuzitatua ili kuendelea kutoa huduma bora katika uwanja huo.

“Kulipa kodi za majengo hapa ni suala la lazima, hivyo ifikapo Septemba mwishoni nataka kuona wafanyabiaashara wote mmeshalipa kodi ya pango, makusanyo haya ni muhimu kwetu ili tuendelee na hatua nyingine za uboreshaji wa viwanja vya ndege na huduma nyinginezo,” alisisitiza Profesa Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Kuhakikisha mikataba yote ya upangishaji wa majengo inapitiwa upya na kufanyiwa marekebisho ili thamani ya fedha iendane na wakati huu.

Profesa Mbarawa amewahimiza wafanyabiashara hao kubadilika na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ili kuweza akuendana na ushindani wa kibiashara uliopo ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri kwa wafanyabiashara nchini ili waweze kufanya biashara zao ili kujiingizia kipato  binafsi na kukuza pato la Taifa.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua sehemu ya kuingilia abiria katika uwanja huo ambapo amesema Serikali itaweka mpango maalum wa muda mfupi kwa wasafiri wanaoenda nje kutotumia muda mrefu katika ujazaji wa fomu wakiwa uwanjani hapo.

“Kwa kushirikiana na taasisi zote zinazotoa huduma katika uwanja huu tutaweka  mpango maalum utakaowezesha wasafiri kuhudumiwa kwa haraka na kwa muda mfupi, Msafiri yoyote anataka huduma za haraka ili waweze kuwahi na sisi tutahakikisho tunakidhi mahitaji ya wateja,” alisema Profesa Mbarawa.

Kwa upande Kaimu MKurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi amesema Mamlaka imeshapitia mikataba yote ya wafanyabiashara kiwanjani hapo na hatua inayofata ni kufatilia madeni yote ili kuboresha huduma katika kiwanja hicho.

Bwa. Msangi ameongeza kuwa kwa yale madeni ambayo hayataweza kulipwa kwa wakati taratibu za kisheria zitafuatwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad