Watuhumiwa wa Mauaji Wafaririki Wakiwa Mahabusu

WATU wanane kati ya 17, wanaotuhumiwa kuua kwa kutumia mapanga, wamekufa mahabusu. Mwendesha Mashtaka, Jonas Kaijage, ameiambia Mahakama ya Wilaya ya Musoma inayosikiliza kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, ambayo watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana mahakama kukosa mamlaka ya kuisikiliza, wanadaiwa kuwaua watu 17 wa familia moja mnamo Februari 16, 2010, eneo la Mugaranjabo, nje kidogo ya mji wa
Musoma.

Kaijage alidai mbele ya hakimu Richard Maganga, kwamba waliofariki wakiwa mahabusu, walimuua Kawawa Kinguye na wenzake16, ambao wote ni wa familia moja kwa kuwakata kwa mapanga.

Aidha, alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa, Sura Bukaba Sura, maarufu Phinias Yona au Epoda (35), aliyetoroka ameunganishwa katika kesi hiyo baada ya kutiwa mbaroni.

Akisomewa mashtaka 17 ya mauaji ya watu hao, Kaijage, alidai mtuhumiwa na wenzake 16, wote wakazi wa wilayani humo, walitenda makosa hayo.

Kaijage alidai kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 18, mwaka huu, akituhumiwa kwa kesi nyingine ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika eneo la Rwamulimi mjini Musoma.

Alidai katika tukio hilo, mtuhumiwa alivamia nyumbani kwa mwananchi mmoja, alivunja nyumba kwa kutumia nondo na kuiba Sh. 500,000.

Alidai polisi walimkamata na ndipo walipomtambua kuwa ni mtuhumiwa wa tukio la mauaji ya watu hao 17 lililotokea mwaka 2010.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 7, mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad