Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Ichiro Aisawa, amesema nchi yake inahitajika kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam baada ya kushuhudia changamoto ya foleni wanayokutana nayo wakazi wa jiji hilo.
Aisawa ambaye kwa sasa ni Mbunge huko Japan huyo amesema hayo alipokutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo ambapo ameahidi kuyafikisha yale aliyoshuhudia nchini Tanzania na kuyapeleka kwa Waziri Mkuu wa Japani, Shinzo Abe.
Mbali na ahadi hiyo aliyoitoa kuhusu changamoto ya foleni, Mbunge huyo pia amempongeza rais Magufuli kwa jitihada mbalimbali anazochukua katika kukabiliana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika suala zima la maendeleo.
Kwa upande wake Rais Magufuli, amemshukuru Waziri huyo wa zamani kwa kuja Tanzania na kusema kuwa serikali yake inatambua mchango mkubwa ambao Japan imekuwa ikiutoa katika suala zima la maendeleo na itaendelea kukuza uhusiano wake na nchi hiyo.
Pamoja na hayo mgeni huyo wa Rais Magufuli, alitembelea baadhi ya miradi inayoendelea kujengwa hapa nchini na kampuni za Japani, ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za juu (flyover) wa TAZARA na mradi wa umeme wa Kinyerezi.