Yusuf Manji Aliwahi Kuvuna Bilioni 150 za Serikali Kwa Mwaka Mmoja tu

TAARIFA mpya zilizopatikana hivi karibuni, zimeonyesha namna mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, alivyoweza kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 150 kupitia zabuni mbalimbali za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kwa mujibu wa tangazo la washindi wa zabuni mbalimbali za Tanesco kwa mwaka 2013, Manji; kupitia makampuni yake mbalimbali ya ndani na nje ya nchi aliweza kushinda zabuni hizo kupitia taratibu za Tanesco.

Hizi ni taarifa za karibuni zaidi kueleza namna mfanyabiashara huyo ambaye kwa sasa yuko katika Gereza la Keko kwa tuhuma zisizohusiana na biashara zake na Tanesco, alivyokuwa akishinda zabuni nono za serikali katika miaka ya nyuma.

Kulinganisha na bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha, kiwango hicho alichopata Manji kingeweza kufadhili yafuatayo kwa mwaka wa 2016/2017; kujenga barabara 12 za kiwango na urefu sawa na kipande cha barabara kutoka Chalinze hadi Morogoro, kuajiri manesi 18,000 na ni sawa na asilimia 70 ya kiasi cha fedha ambacho serikali inagharamia kujenga Uwanja wa Ndege mpya jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwa sababu baadhi ya kampuni za Manji zilizoshinda zabuni hiyo zimesajiliwa katika nchi zinazojulikana kama pepo ya wakwepa kodi (Tax Havens), ni vigumu kujua ni kiasi gani cha kodi kililipwa naye baada ya kuvuna mabilioni hayo ya fedha.

Jina la Manji ni miongoni mwa majina ya wafanyabiashara maarufu hapa nchini ambao wamewahi kutajwa na vyombo vya kimataifa kuwa wamehifadhi ukwasi mkubwa katika akaunti zao zilizo nje ya Tanzania.

Raia Mwema/JF
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad