Mshambuliaji wa Mabingwa watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga Ibrahim Ajib amefanikiwa kuitoa timu yake kifua mbele baada ya kuifungia bao moja la pekee dhidi ya Njombe Mji FC mchezo ulipigwa katika viunga vya Sabasaba mkoani Njombe.
Mshambuliaji Ibrahim Ajib.
Bao hilo la Ajib limepatikana kwa mkwaju wa faulo ndani ya dakika 16 za mchezo kipindi cha kwanza na kupelekea mpaka dakika 45 za awali kuisha timu ya Yanga kuwa mbele kwa bao moja.
Pamoja na hayo, timu ya Njombe Mji ilionekana kufanya mashambulizi makali wakati walivyorudi kutoka mapumziko lakini kwa bahati mbaya juhudi zao hazikuweza kuzaa matunda ya aina yeyote kwa siku ya leo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kuisha nahodha wa timu ya Yanga Thabani Kamusoko amesema mechi ya leo kwa upande wao haikuwa rahisi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa waliyokutana nayo huko Njombe.
"Wachezaji wamepambana sana katika mechi ya leo, japokuwa mazingira ya baridi yalitusumbua katika mechi ya leo lakini tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kupata pointi tatu", amesema Kamusoko.
Kikosi cha Yanga
Kwa upande mwingine, Ibrahim Ajib ameweza kujiandikia rekodi yake mpya ya kushinda bao la kwanza katika msimu 2017/2018 ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na wana Yanga.