Chile. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Franco Luis ameshambuliwa na kundi la simba baada ya kujirusha ndani ya bustani ya wanyama hao akiwa uchi.
Luis aliwaacha mdomo wazi watu waliofurika kwenye bustani hiyo ya Santiago mwishoni mwa wiki ambao wengi waliambatana na familia zao.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kijana huyo mwenye miaka 20, alikimbizwa hospitali baada ya walinzi wa bustani hiyo kumuokoa kwa kuwaua simba wawili waliokuwa wanamshambulia.
Uongozi wa bustani hiyo ulithibitisha tukio hilo na kudai kwamba kijana huyo alishambuliwa akiwa uchi wa mnyama baada kuvunja uzio na kuingia kwenye kundi hilo.
Mkurugenzi wa Santiago Alejandra Montalva alisema walijua kijana huyo aliingia kwenye bustani hiyo kama wateja wa kawaida wanavyolipa tiketi kwa lengo la kutembelea hapo.
‘‘Baada ya kufanya malipo kama mteja wa kawaida kijana huyo hakupita kwenye njia inayotumiwa na wateja bali aliezua paa la simba hao na kutumbukia ndani na kuanza kushambuliwa,’’ alisema
Alisema ni kitendo cha kushangaza kwani kila mtu alishikwa na bumbuwazi baada ya kumuona kijana huyo akijirusha kwenye kundi hilo la simba na kuanza kupigana nao.
Alisema askari wa bustani hiyo walitumia nguvu za ziada kuhakikisha wanaokoa maisha ya kijana huyo, ambaye hawajafahamu fika kama alikuwa na akili timamu.
Atoa sababu
Kwa upande wake kijana huyo alisema alifanya kitendo hicho cha kustaajabisha kila mtu kutokana na ufunuo alioshushiwa na Mungu.
Shuhuda
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Cynthia Vasquez alisema baada ya Luis kujirusha ndani ya bustani hiyo, simba waliokuwa ndani hawakumdhuru kwanza.
“Cha kushangaza simba hao walianza kucheza naye,”alisema Vasquez
Vasquez ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waliotembelea bustani hiyo, alisema baada ya dakika chache Lius alisikika akipiga kelele. “Walianza kumrarua...alipiga kelele aliita jina la Yesu,”alisema.
Alisema kelele hizo ziliwavuta watu wengi ambao walifika kushuhudia tukio hilo.
Vasquez alisema walinzi waliofika kuokoa maisha ya Luis walilazimika kufyatua risasi juu ili kuwatawanya watu. “Waliingia baada ya kuwaua simba hao na kumtoa Luis ambaye alikuwa ameshajeruhiwa vibaya,” alisema.
Baba aongea
Baba mzazi wa Luis alisema alishaanga kusikia watu wanapiga kelele na alipofika katika eneo la tukio alimkuta kijana wake akiwa amejeruhiwa vibaya na simba.