Changamoto ya Upungufu wa watumishi Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala imeelezwa kuwaelemea watoa huduma hali inayoathiri huduma hospitalini hapo.
Hali hiyo imetokana na watumishi wakiwamo wauguzi 50 kuondolewa hospitalini hapo baada ya kubainika kuwa na vyeti feki.
Hayo yamebainika leo, wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliyetembelea hospitali hiyo kwaajili ya kukagua miundombinu pamoja kuzungumza na watumishi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Daniel Nkungu amesema, Hospitali hiyo ina watumishi 300 huku ikiwa na upungufu wa watumishi 200 hasa manesi na wauguzi.
"Wakati Hospitali hii inajengwa mwaka 1973 ilikuwa inatoa huduma kwa watu wachache lakini kumekuwa na ongezeko kubwa la watu hasa wajawazito na watoto," amesema
Amesema, idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na wagonjwa 2500 wanaofika kila siku Hospitalini hapo kwaajili ya kupata huduma.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ameahidi kufikisha suala hilo kwa Wizara ya Utumishi pamoja na Waziri wa Fedha kwaajili ya kuomba kuongeza watumishi hospitalini hapo.
"Inawezekana Vituo vyote vinakuwa treated bila kuzingatia idadi ya watu na mahitaji, mimi nimeona kuna shida," amesema Hapi
"Hospitali ya Mwananyamala inaweza ikawa inahudumia watu wengi kuzidi Hospitali ya Rufaa ya Bugando, tutaendelea kuwashauri viongozi wetu ili kwa sisi ambao tuna idadi kubwa ya watu tuongezewe watumishi," amesema Hapi
Aidha, amewataka kusimamia matumizi ya dawa na zinazotolewa na Bohari ya dawa(MSD) na kuonya watumishi wenye tabia ya kuziuza kwa wagonjwa