Asilimia 60 ya mashuka ya hospitali ya Wilaya ya Kinondoni ya Mwananyamala yamedaiwa kupotelea Muhimbili.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Festo Duganga alisema hayo leo wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya hiyo hospitalini hapo.
Amesema, ukosefu wa mashine za kufulia mashuka unasababisha kutumia Sh16milioni kwa mwezi kutokana na kutumia mashine za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
"Mashuka yetu tunapeleka kufua Hospitali ya Muhimbili, lakini asilimia 60 ya mashuka hayarudi kwakuwa si rahisi kuyatambua," amesema Dk Duganga
Dk Duganga amesema licha ya changamoto nyingi, Hospitali hiyo imefanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh25milioni hadi Sh30milioni kwa wiki.
Amesema, kiasi hicho cha fedha kinatokana na malipo ya huduma kupitia michango pamoja na bima ambapo asilimia 70 hutumika kwa ajili ya kununua vifaa tiba pamoja na dawa huku asilimia 30 kwa ajili ya maboresho ya miundombinu.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Daniel Nkungu alisema, Hospitali hiyo ina watumishi 300 huku ikiwa na upungufu wa watumishi 200 hasa manesi na wauguzi ambao wanahitajika kukidhi mahitaji.
"Wakati Hospitali hii inajengwa mwaka 1973 ilikuwa inatoa huduma kwa watu wachache lakini kumekuwa na ongezeko kubwa la watu hasa wajawazito na watoto," amesema
Amesema, idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na wagonjwa 2500 wanaofika kila siku hospitalini hapo kwaajili ya kupatiwa huduma hali inayosababisha watumishi waliopo kufanya kazi zaidi ya muda wao wa kazi.
Mkuu wa Wilaya hiyo Ally Hapi alisema ni kweli uhakiki wa vyeti umeleta athari kwenye Hospitali nyingi ikiwamo ya Mwananyamala huku akiahidi kufikisha suala hilo kwa Wizara ya Utumishi pamoja na Waziri wa Fedha kwaajili ya kuomba kuongeza watumishi hospitalini hapo.
"Inawezekana Vituo vyote vinakuwa treated bila kuzingatia idadi ya watu na mahitaji, mimi nimeona kuna shida," amesema
"Hospitali ya Mwananyamala inaweza ikawa inahudumia watu wengi kuzidi Hospitali ya Rufaa ya Bugando (Mwanza),lakini tutaendelea kuwashauri viongozi wetu ili kwa sisi ambao tuna idadi kubwa ya watu tuongezewe watumishi," amesema Hapi
Aidha, aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kusimamia vizuri matumizi ya dawa zinazotolewa Bohari ya dawa (Msd) huku akiwaonya baadhi ya watumishi wenye tabia ya kuziuza kwa wagonjwa.