Kuripoti kwa askari huyo kunatokana na agizo alilolitoa jana Jumapili, Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Peter Sima awe amempeleka leo Jumatatu baada ya kutuhumiwa na wananchi wa Mbagala kwamba amekuwa akidai rushwa.
Kamanda Mambosasa pia ametoa wiki moja kwa Kaimu Kamanda Sima awe amefuatilia tuhuma za rushwa zilizowasilishwa kwake na wananchi.
Amesema askari huyo ataendelea kufuatiliwa ili kubaini ukweli wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake na endapo zitathibitishwa taarifa zitawasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na atachukuliwa hatua za kisheria.
“Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke alimleta huyu askari ambaye nimemuhoji na kumruhusu kuendelea na kazi wakati akiendelea kuchunguzwa ndani ya wiki moja,” amesema Kamanda Mambosasa.
Akizungumza na wakazi wa Mbagala, walilalamika wakidai askari huyo anayejiita Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara na kudai kwa nguvu rushwa ya Sh20,000.
Wananchi hao wamelalamika kuwa, mfanyabiashara ambaye hatoi fedha hizo hufungwa pingu na kuzungushwa usiku kucha akiwa kwenye gari la polisi.
Kamanda Mambosasa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi wa Mbagala Zakhem alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari anayejipa jina la mzaha, huku akiwakandamiza wananchi.