SIKU moja baada ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupiga marufuku kutumika kwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam uliopo katika matengenezo, mechi ya Simba na Yanga sasa itachezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mechi hiyo itachezwa Oktoba 28, mwaka huu na awali ilielezwa ingechezwa kwenye Uwanja wa Taifa ambao ulielezwa ukarabati wake ungekamilika Oktoba 25, mwaka huu.
Hivi karibuni serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ilisema Simba na Yanga hazitaweza kuutumia Uwanja wa Taifa kwa mechi ya Oktoba 28 kwani ukarabati wake utakuwa bado haujakamilika.
Kikosi cha timu ya Simba.
Badala yake serikali ikasisitiza kwamba, uwanja huo utakuwa tayari kuanza kutumika ifikapo Januari mwakani.
Kwa jinsi hali ilivyo, Tanzania hakuna uwanja mwingine wa kuruhusu mechi hiyo kuchezwa zaidi ya Kirumba ndiyo maana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litalazimika kuipeleka huko.
Mechi hiyo ya watani itachezwa kwenye uwanja huo kama ilivyopangwa Oktoba 28, mwaka huu.
“Unadhani hii mechi itapelekwa wapi? Hapa Tanzania hakuna uwanja mwingine utakaoweza kuchukua watazamaji wengi kama Kirumba hivyo kwa vyovyote vile mechi itachezwa hapo,” kilisema chanzo chetu.