Bado Najisikia Uzito Kueleza Jamii Hali ya Lissu Mwili Wake Umevunjwa Vunjwa- Mashinji

 Bado Najisikia Uzito Kueleza Jamii Hali ya Lissu Mwili Wake Umevunjwa Vunjwa- Mashinji
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji amefunguka na kudai anajisikia uzito kuelezea hali ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu inavyoendelea huku akimtaka aliyefanya kitendo hicho ajitafakari.

Katibu Mkuu wa chama cha Kidemokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji.
Mashinji ametoa kauli hiyo leo asubuhi wakati CHADEMA ikitoa msimamo wake na kuelezea hali ya Mbunge huyo wa Singida Mashariki ambaye bado anapatiwa matibabu nchini Kenya kufuatia kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge huyo.

"Bado najisikia uzito wa kuelezea jamii ya Watanzania hali ya kiongozi wetu Tundu Lissu, najua nina jukumu kubwa kama mtendaji wa chama kutaarifu umma juu ya hali ya Lissu inavyoendelea. Ni majonzi makubwa sana na kama kuna mtu katika taifa hili alifanya hicho kitendo anatakiwa ajitafakari sana. Mpaka jana asubuhi ameenza kupatwa na matatizo ya kifua kutokana na kulala kitandani muda mrefu, na kwa sababu mguu wake wa kulia umevunjwa vunjwa kwa risasi, nyonga yake pia mkono wake umevunjwa kwa risasi lakini 'inshallah' kama nilivyosema awali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeamua kuchukua roho ya nani na aache ya nani", amesema Mashinji.

Aidha, Mashinji amesema wamemuumiza sana Lissu ila hawataacha kumpigania ili aweze kupona na kutoka katika hali aliyokuwa nayo kwa sasa ili aweze kurudi kuendelea kuwapigania Watanzania.
"Waswahili wanasema hujafa hujaumbika, kwa kweli wamemuumiza kwa hiyo ndugu zangu hiyo hali ya Lissu jana ilikuwa mbaya mpaka wakamuwekea mipira ya kupumulia lakini ilipofika wakati wa mchana hali yake ilikuwa inaendelea vizuri. Tunasafari ndefu ya kuhakikisha Lissu anapona, sasa hivi wamemtibu zile sehemu za ndani ambazo zingeweza kuhatarisha maisha yake kwa zile risasi zilizopita tumboni na sehemu nyingine", amesema Mashinji.

Pamoja na hayo, Mashinji ameendelea kwa kusema "Mhe. Lissu ni kweli tuliambiwa alipigwa risasi tano katika mwili wake lakini kulingana na hali ya mwili ulivyobomolewa yawezekana zilizidi. Leo ni siku ya tano akiwa anatibiwa hospitali na mpaka sasa hivi ameshafanyiwa oparesheni tatu nadhani itabidi kuzisitisha kidogo ili kumpa ahueni aweze kupumzika na yeye. Tulitegemea ingekuwa suala la kawaida tu yeye kwenda kutibiwa na kurudi lakini imekuwa tofauti. Msilie wala kusononeka kwa sababu Lissu bado yupo hai anaendelea kupigana na sisi, kuhakikisha kwamba anapona na kurudi kuendeleza ukombozi Watanzania ili kufikia uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli", amesisitiza Mashinji.

Kwa upande mwingine, Mashinji amesema wanajiandaa kisaikolojia kumpokea Lissu na hali ambayo atarudi nayo kwa kuwa hiyo ndiyo zawadi waliyopewa na Mwenyezi Mungu.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad