Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha) limesema licha ya takwimu kuonyesha kwamba maambukizi ya VVU yanapungua nchini bado wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari.
Takwimu za Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) zinaonyesha maambukizi yalipungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012.
Akizungumza leo, Mratibu wa Kanda ya Dar es Salaam wa Nacopha, Edna Edson amesema wananchi wasibweteke na kupungua kwa maambukizi bali wachukue hatua kukabiliana na virusi.
Amewaeleza waratibu wanaopata mafunzo ya kusimamia ruzuku ya mradi wa Sauti yetu unaoendeshwa na baraza hilo kwamba elimu kwa wananchi ndiyo suluhisho katika kukabiliana na maambukizi mapya.
Amesema mradi huo utatekelezwa kwenye halmashauri 46 nchini huku ukilenga kuelimisha jamii ili ione sababu za kutafuta ushauri na upimaji wa virusi vya Ukimwi.
“Mradi huu pia unalenga kuelimisha jamii ya watu wanaoishi na VVU ili kuongeza upatikanaji wa huduma na kuhakikisha wanaendelea kupata tiba,” amesema na kulishukuru Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kwa kufadhili mradi huo.
Baadhi ya halmashauri utakakotekelezwa mradi huo ni pamoja na Temeke, Kilombero, Lindi, Korogwe Morogoro na Masasi.
Kwa upande wake, Daisy Majamba aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kama hatua hazichukuliwi Ukimwi unaweza kuleta athari katika jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Mradi huu na elimu itakayotolewa itamfanya kila mmoja wetu kupata uelewa na hivyo kujikinga na maambukizi,” amesema.
Ametaka uongozi wa baraza hilo kutekeleza mradi huo na kuhakikisha kwamba unawafikia walengwa ili jamii nzima ya watanzania iweze kunufaika.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nacopha, Deogratius Rutatwa aliwataka waratibu hao kuzingatia mafunzo ili ruzuku zitakazotolewa kwa ajili ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.