Wito uliotolewa Julai 20 na Rais John Magufuli na Pierre Nkurunziza wa Burundi wakiwa mkoani Kagera kuwataka wakimbizi kwenda kuijenga nchi yao kutokana na usalama kuimarika, umeanza kutafutiwa fedha kutoka jumuiya ya kimataifa.
Katika kutekeleza mpango huo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema linahitaji Dola 3.7 milioni za Marekani (zaidi ya Sh8.2 bilioni) kuwarudisha nyumbani Warundi walioonyesha nia ya kufanya hivyo.
IOM imesema itashirikiana na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) kufanikisha suala hilo baada ya wakimbizi 12,000 kuridhia kurudi nyumbani ambako taarifa zinasema usalama umeimarika.
Mkakati wa kuwarudisha wakimbizi hao waliowasili nchini tangu Aprili 2015 unatekelezwa baada ya mkutano uliofanyika Agosti 31 na kuwakutanisha maofisa wa Serikali za Tanzania, Burundi na UNHCR kupitisha mpango huo.
Kwa mujibu IOM, mambo kadhaa yaliridhiwa kwenye mkutano huo ikiwamo kufanikisha kuwarudisha kwa awamu wakimbizi 12,000 walio tayari kuanzia Septemba 7 mpaka Desemba 31. “IOM inao utaalamu wa kutosha kuwasafirisha wakimbizi kwa kuwapa mahitaji yote muhimu vikiwamo vipimo vya afya kabla ya kuanza safari,” inasema taarifa IOM.
Katika ushirikiano huo, IOM imedai UNHCR inatakiwa kufanikisha usafiri wao kutoka kambi za Nyarugusu na Mtendeli mpaka ile ya Nduta ambayo ni kituo cha kuondokea nchini. Mikoa 10 imeandaliwa nchini humo kuwapokea wakimbizi wanaorudi, mikoa hiyo ni Ruyigi, Muyinga, Makamba, Kirundo, Rutana, Cankuzo, Karuzi, Bujumbura, Rumonge na Ngozi.