MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Alhaji Abdallah Bulembo amejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Novemba mwaka huu.
.
Bulembo alikuwa ni miongoni mwa makada 49 wa CCM waliochukua fomu za kuwania uenyekiti wa taifa akitaka kutetea nafasi yake, lakini sasa ameamua kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Kwa kauli yake anasema; “Uamuzi huu nimeufikia baada ya kuona kwamba katika kinyang’anyiro hiki kwenye nafasi ya uenyekiti tulijitokeza wagombea 49. Sasa nina uhakika baada ya kujitoa mimi katika 48 waliobaki lazima atapatikana CCM ambaye viatu vyangu vitamtosha,”
Mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake akasema kuwa ameamua kutogombea sio kwa shinikizo lolote kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ndani ya chama hakuna sehemu yoyote inayomzuia kuwania uongozi.
Akasema kuwa anafurahi kwamba anaiacha Jumuiya hiyo ikiwa bora kuliko alivyoikuta, akisema, kwamba sasa hadhi ya shule za jumuiya hiyo imepanda kitaaluma, na pia jumuiya imeweza kulipa asilimia 68 ya madeni aliyokuta ikidaiwa.
Hayo ndiyo yalikuwa maelezo ya Bulembo wakati akitangaza hatua yake ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho wiki iliyopita alipokutana na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari, jijini Dar es Salaam.
Ni kweli juhudi ambazo Bulembo amezifanya, ili kuhakikisha jumuiya hiyo inarudi kwenye hadhi kama ilivyokuwa zamani ni kubwa, hivyo mwenyekiti mpya atayechaguliwa ni vyema aendeleze pale Bulembo alipoishia.
Siyo siri kwamba amejitahidi kufanya mchakato wa kurejesha mali za jumuiya hiyo, ambazo zilikuwa zinamilikiwa na baadhi ya watu ikiwamo Shule ya Sekondari Kaole ya mjini Bagamoyo mkoani Pwani ingawa alikumbana na changamoto nyingi.
Mbali na hayo, baadhi ya shule zilishindwa kulipa mishahara ya watumishi kwa wakati muafaka hali iliyodhoofisha utendaji kazi katika jumuiya husika hadi ikafikia kuwapo uvumi wa kurudishwa shule hizo mikononi mwa serikali, lakini akawa ameziimarisha kufuatia baadhi kuendeshwa kama mali ya mtu binafsi.
Kwa maelezo zaidi ya Bulembo ni kwamba katika uongozi wake aliikuta akaunti ya jumuiya ikiwa haina kitu, lakini sasa ina fedha ambayo ataikabidhi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa taifa.
Aidha, akasema kuwa chini ya uongozi wake amefanikiwa kupima viwanja 56,000 vya jumuiya ya wazazi na hivyo kuiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kimaendeleo.
Lakini mbali na hayo, Jumuiya hiyo pia iliwahi kukunjua makucha na kuwatangazia mafisadi waliovamia viwanja vyake kuvisalimisha mara moja vinginevyo wangenyang'anywa kwa nguvu.
Kwamba kamwe mali zake haziwezi kuendelea kuwa `shamba la bibi.'
Kwa mtazamo wangu nikiuangalia uongozi wake ninaona kwamba hata kama hakufanikiwa kurejesha mali zote mikononi mwa jumuiya, lakini juhudi zake zilionekana.
Hizo ni pamoja na kukemea vitendo vyote vyenye lengo la kuivuruga jumuiya hiyo.
Hivyo wakati huu ambapo jumuiya inajiandaa kufanya uchaguzi ni vyema kiongozi ajaye aanzie pale Bulembo alipoishia, ili kuendeleza mapambano ya kukomboa mali za jumuiya, ambazo bado ziko mikononi mwa watu wachache.
Ninajua wapo makada wengi wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao baadhi yao ni Dk. Edmund Mndolwa, Mtiti Butiku, Daud Manoti, James Ouma, Simon Rubugu, David Msuya, Vitus Lipagile, Japheti Kasiri, Maliki Maruru na Paul Chacha.
Wengine ni mwenyekiti wa zamani wa jumuiya hiyo, Abiud Maregesi, Burton Kihaka, Jafari Kunambi, George Busungu, James Albert, George Nangale, Malila Malila, Semmy Kiondo, Levina Lemomo, Dk. Walter Nko, John Lema na Israel Salufu.
Wapo pia Frey Msekeni, Ali Makwilo, Manfred Lioto, Swalehe Katala, Dk. Damas Kashegu, Richard Lugandu, Jacob Mzuri, Nicholas Haule, Deogratius Magongwe, Kanuth Ndagine, Geofrey Sanga, Fatma Kasenga, Adam Malima, Charles Maguye, Mohamed Mgoli na Abednego Range.
Kwa hali hiyo ni muhimu wanachama kuwapima na kuchagua kiongozi atakayeendeleza alikoishia Bulembo.
Novemba mwaka 2012, Jumuiya hii ya Wazazi ilifanya uchaguzi wa viongozi wake wa taifa na kumchagua Alhaji Bulembo kushika nafasi hiyo ambayo sasa ameona awaachie makada wengine wa CCM.
Nakumbuka katika uchaguzi Bulembo alipata kura 673 akifuatiwa na Martha Mlata aliyepata kura 107, huku John Barongo, ambaye kwa sasa ni marehemu akiwa amepata kura 51.
Baada ya ushindi huo wapo baadhi ya watu waliandika kwenye mitandao ya kijamii wakibeza uwezo wa Bulembo na kudai kuwa hana lolote na hawezi kuisaidia jumuiya hiyo wala CCM kupiga hatua.
Lakini sio siri kwamba amefanya makubwa hadi kufikia kuvalishwa vazi aina ya Mpuzu la heshima kwa kabila la Waha na kutawazwa kuwa kiongozi anayeheshimika, alipokuwa katika ziara ya kichama mkoani Kigoma.
Mwenyekiti huyo amefanya kazi kubwa ikiwamo kuimarisha jumuiya kama ambavyo alieleza alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kujitoa kuwania nafasi hiyo na pia ameingiza wanachama wapya ndani ya CCM.
Juni 10 mwaka huu alihitimisha ziara yake ya kichama akiwa amefanikiwa kutembelea mikoa saba na jumla ya wilaya 47 za mikoa husika, ziara ambayo ilianza Mei 26 mwaka huu akiwa 'amezoa' wanachama wapya 376.
Jumuiya ya Wazazi ya CCM, ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Tanzania Parents Association (TAPA) ilianzishwa mwaka 1955 na sasa ina umri wa miaka 62 ikiwa imeongozwa na makada mbalimbali wa chama hicho.
Baadhi ya makada hao ni Idd Simba, Abiud Maregesi, Athman Mhina na Bulembo, ambaye sasa ametangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo na kuwaachia wengine