Bunge limelazimika kutoa taarifa hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa hospitali ya Nairobi mbaka jana ilisema haijapokea fedha hizo kutoka kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ofisi ya Bunge inapenda kusisitiza kuwa fedha zilizochangwa na Wabunge kiasi cha Tsh. Milioni 43 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Mheshimiwa Tundu Lissu tayari zimetumwa katika Akaunti ya Hospitali ya Nairobi anakopatiwa matibabu. Fedha hizo zimetumwa kupitia Benki kuu ya Tanzania (BOT) ambapo kwa mujibu wa viwango vya kubadilishia fedha vya BOT kwa siku hiyo ilikuwa ni sawa na Shilingi ya Kenya 1,977,120.58." ilisema taarifa ya Bunge
Taarifa hiyo ya Bunge iliendelea kusisitiza kuwa walituma fedha hizo Septemba 20, 2017
"Kiasi hicho cha Fedha kilitumwa siku ya tarehe 20 Septemba, 2017 kwenda Benki ya Barclays, Tawi la Hurlringham, Akaunti Namba 0451155318 yenye jina la Kenya Hospital Association"
Septemba 22, 2017 Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alisema kuwa mbaka siku hiyo anatoa taarifa mbalimbali kuhusu Tundu Lissu fedha ambazo wabunge walikuwa wamechanga kwa ajili ya matibabu ya Tundu Lissu zilikuwa hazijafika Hospitali Nairobi Kenya, lakini siku moja baadaye Bunge lilitoa taarifa na kusema walikuwa wameshatuma fedha hizo toka Septemba 20 mwaka huu, baadaye zikawepo taarifa kutoka hospitali ya Nairobi kuwa bado hawajapata fedha hizo kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.