CUF ya Maalim Seif Imeipongeza Kambi ya Upinzani Kususia Kuapishwa Wabunge Wapya

CUF Upande wa Maalim Seif Umeupongeza Kambi ya  Upinzani Kususia Kuapishwa  Wabunge Wapya
Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad umepongeza uamuzi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kususia kuapishwa wabunge wapya wa viti maalumu wa chama hicho.

Wabunge walioapishwa jana Septemba 5 wanachukua nafasi ya wenzao waliofukuzwa uanachama na Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa CUF, Mbarala Maharagande amesema leo Septemba 6 kuwa bado wanawatambua wabunge wanane waliovuliwa uanachama hivyo kupoteza ubunge.

Amesema Baraza Kuu la Uongozi la CUF linaendelea kuwatambua wabunge na madiwani waliovuliwa uanachama kwa kuwa bado ni wanachama halali wa chama hicho.

Maharagande amemtupia lawama Spika Job Ndugai akidai analitumia Bunge vibaya kukandamiza upinzani.

Amesema bunge linapaswa kuwa chombo muhimu cha Watanzania katika kuisimamia Serikali ili wananchi wapate maendeleo.

Spika Ndugai jana aliwaapisha wabunge saba wa viti maalumu ambao ni Alfredina Kaigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.

Hindu Mwenda, ambaye pia alikuwa aapishwe jana alifariki dunia Ijumaa Septemba Mosi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuzikwa Jumapili Septemba 3.

Wakati wabunge wa upinzani wakisusia, waliohudhuria ni wabunge wa CUF Magdalena Sakaya wa Kaliua, Maftah Nachuma (Mtwara Mjini) na Maulid Mtulia (Kinondoni).

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad