Deni Linalotokana na Gharama za Matibabu Nje ya Nchi Lafikia Bilioni 35

Deni Linalotokana na Gharama za Matibabu Nje ya Nchi Lafikia Bilioni 35
Serikali imesema deni linalotokana na gharama za matibabu nje ya nchi limefikia Sh35 bilioni na kuitaka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhakikisha inatoa rufaa kwa kuzingatia taratibu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutibu magonjwa ambayo yanaweza kutibiwa ndani ya nchi kwa kuwa imeshasomesha wataalamu wa kutosha na kwamba vifaa pia vipo.

Ummy alisema nchi imekuwa ikitumia Sh5 bilioni kila mwaka kwa ajili ya matibabu nje na kwamba magonjwa ya saratani na upandikizaji wa vifaa vya usikivu yanaigharimu zaidi Serikali.

“Hivi sasa deni la matibabu nje ya nchi linafika Sh35 bilioni na hilo ni deni la miaka minne iliyopita,” alisema Ummy.

“Kwa sasa tumepunguza kwa kuwa wale ambao tulikuwa tunawapeleka nje kwa ajili ya kwenda kuwekewa vifaa vya usikivu ambao tulikuwa tunatumia zaidi ya Sh2 bilioni kwa mwaka, sasa tunafanyia ndani ya nchi hatutumiia fedha nyingi,” alisema Ummy.

Kuhusu matibabu nje ya nchi, Ummy alisema Serikali haijazuia wagonjwa kupelekwa nje ikiwa wana uwezo wa kujigharimia.

Ummy alisema utaratibu wa wagonjwa kusafirishwa ulibadilishwa.

“Zamani wizara ndiyo ilikuwa inatoa rufaa, siku hizi hatutoi mpaka tupate taarifa ya daktari ya Muhimbili, MOI, JKCI au Ocean Road. Waseme hatuwezi na tukishapata hiyo taarifa sasa ndiyo tunasema sawa tutampeleka,” alisema Ummy.

“Wenye fedha zao binafsi hatuwezi kuwazuia, tunasema wale ambao wanataka kugharamiwa na Serikali.”

Waziri Ummy aliwatahadharisha wataalamu hao na wanasiasa kwamba lazima wahakikishe kweli hawawezi kutibu na kwamba Wizara ipo tayari na itawaunga mkono.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru alisema wapo tayari kutibu magonjwa yote yanayowezekana hapa nchini na hilo litafanikiwa ikiwa watakuwa na rasilimali watu na vifaa vya kutosha.

Alisema Muhimbili imeanza kuchukua hatua baada ya kuanza kutoa huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu Juni mwaka huu.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na kujenga uwezo wa ndani kwa kusomesha watu na kuwekeza kwenye vifaa.

“Tunatarajia hivi karibuni kuanza upandikizaji wa figo kwa kuwa ni ugonjwa ambao Serikali imekuwa ikipeleka nje wagonjwa wengi kwa matibabu na kwamba utaratibu wa maandalizi umefikia tamati,” alisema.

“Hivyo tutakuwa tunawekeza kwenye vifaa na rasilimali watu ili kuendana na azma ya Serikali ili wagonjwa watibiwe hapa nchini kadri inavyowezekana . Hatusemi kwamba tutatibu wote, kwa wengine vitahitajika vifaa na ujuzi zaidi ambao hatuna.”

Wakati huohuo, Ummy amepokea msaada wa vifaa vipya kwa ajili ya vyumba viwili vya upasuaji watoto wadogo na wodi ya watoto ya upasuaji vyenye thamani ya dola 675,000 za Kimarekani (awa na Sh1.5 bilioni), vilivyotolewa na taasisi ya Archie Wood Foundation ambayo ni ya wataalamu na wahisani kutoka Uingereza.

Kwa upande wake Profesa Museru alisema msaada huo utasaidia vyumba vya upasuaji watoto.

“Kuna vifaa mbalimbali kama taa za kufanyia upasuaji, vitanda, mashine za usingizi na monitor zake, mashine za kuzuia damu kupotea wakati wa upasuaji, mashine ya kusafisha vifaa vya upasuaji na vifaa vyake,” alisema Profesa Museru.

Alisema msaada huo utawezesha kitengo cha upasuaji wa watoto kuwa na vyumba viwili vya upasuaji ambavyo vimekamilika na vyenye vifaa vya kisasa hivyo upasuaji utafanyika mara 10 kwa wiki badala ya ya mara tatu kwa wiki.

Akikabidhi msaada huo, mshauri mwelekezi wa taasisi hiyo, Profesa George Youngson alisema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia MNH katika kutoa huduma za hali ya juu ili kupunguza rufaa zisizokuwa za lazima.

Alisema wataendelea kutoa msaada wa vifaatiba na ikiwezekana kuleta wataalamu nchini kufanya upasuaji ili kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad