Diwani Mwingine wa Chadema Arusha Aachia Ngazi Mbele ya JPM


Katika hali ambayo haikutarajiwa, Diwani wa Kata ya Kimandolu Jiji la Arusha (Chadema), Mchungaji Rayson Ngowi akiongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametangaza kumuunga mkono Rais John Magufuli na kwa kuachia nafasi yake.

Alifanya hivyo jana mbele Rais Magufuli wakati madiwani 10 wa Chadema waliojiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti kwenye halmashauri tatu za Arusha na kujiunga na CCM walipoitwa wakati Rais alipokuwa akihutubia baada ya kutunuku kamisheni kwa maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Hatua hiyo inafanya jiji la Arusha linaloongozwa na Chadema kupoteza kata mbili.

Madiwani wengine waliojitambulisha mbele ya Rais Magufuli ni wale waliojiuzulu katika halmashauri za Meru na Arusha Vijijini.

Mchungaji Ngowi ndiye aliyekuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuanza kumwagia sifa Rais Magufuli, “Mwanzoni nilikuwa sikuelewi lakini sasa nakuelewa sana. Nataka Watanzania wote wakuunge mkono. Tunaona jitihada zako za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya asali na maziwa. Tuko pamoja na nashukuru sana kwa kunipokea.”

Mwingine aliyepanda jukwaani ni aliyekuwa Diwani wa Muriet, Credo Kifukwe ambaye alisema,

Nimeamua kumuunga mkono Magufuli kutokana na kazi nzuri alizofanya na kila mwenye akili timamu anaona. Huko tulikokuwa ilikuwa mambo ya pingapinga hawataki kuona mazuri yanayoendelea, nimeamua kurudi CCM hapa kazi tu.”

Baadaye Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema, “Hawa wananchi wanataka maendeleo kuliko majina ya vyama na maendeleo hayajali wewe ni CCM , Chadema au CUF.”

Hata hivyo, alionyeshwa kushangazwa na madiwani hao kuacha haki zao zikiwamo masilahi mengine na kuamua kujizulu nafasi zao na kuwakaribisha CCM.

Pia, aliutaka uongozi wa CCM kuwapitisha madiwani hao kuwania tena nafasi hizo ili wakashindane na vyama vingine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad