Hawa Ghasia Alilia Tohara kwa Wanaume Kilazima

Hawa Ghasia Alilia Tohara  kwa Wanaume Kilazima
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia ameiomba serikali ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kutoa huduma ya tohara kwa wanaume kilazima ili iweze kusaidia kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Mhe. Ghasia ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anauliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kusema ni serikali inapata kigugumizi gani katika suala la tohara kwa wanaume lisiwe la lazima kama yaliyovyo magonjwa mengine yanayotolewa chanzo katika vituo vya afya.

Kutokana na hayo, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla amemjibu kwa kusema serikali haipati kigugumizi chochote juu ya jambo hilo kwa kuwa ni la hiyari na wala siyo lazima.

"Kwanza kiujumla ni lazima ieleweke dhana ya ridhaa kwenye huduma za afya na tiba kwa sababu ni jambo la hiyari kama vile ilivyo kwa matibabu mengine yote ni lazima mtu atoe ridhaa yake ndipo aweze kupatiwa huduma ya kufanyiwa tohara na haiwezi hata siku moja kuwa ni jambo la lazima. Na kwa msingi huo serikali haina kigugumizi chochote juu ya hilo", amesema Dkt. Kigwangalla.

Pamoja na hayo, Dkt. Kigwangalla ameendelea kwa kusema "Nichukue nafasi hii Mhe. Spika kutoa rai kwa wakina mama wote nchini kutumia fursa  ya kuwashawishi wenza wao kwa kuzungumza nao kwa upole, heshima na upendo wa hali ya juu ili wale ambao hawajafanya tohara waende kwa hiari yao katika vituo vya afya waweze kutahiriwa", amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande mwingine, Dkt. Kigwangalla amesema tohara inapunguza maambukizo ya Virusi Vya Ukimwi (VVU)kwa asilimia 60 hivyo amewataka wanaume wote ambao bado hawajafanyiwa tohara kutumia nafasi hiyo kwenda kwenye vituo vya kutoa huduma hiyo ili waweze kupewa huduma hiyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad