KATIKA kuhakikisha timu yake inapata ushindi kwa kutumia mipira ya pembeni, Kocha wa Yanga, George Lwandamina amemuongezea mbinu beki wake wa kulia, Juma Abdul.
Lwandamina amefanya hivyo katika mazoezi ya timu hiyo wiki hii kuelekea mechi ya leo ya Ligi Kuu Bada dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Abdul ni kati wachezaji wanaotengeneza mabao kutokea pembeni kutokana na kusifika kwa uwezo wake mkubwa wa kupiga krosi, faulo na kona zenye macho kuelekea lango la adui.
Championi Jumamosi, lilikuwepo kwenye mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru karibu wiki hii yote na kuona jinsi Abdul anavyoongezewa mbinu na Lwandamina.
Lwandamina alionekana akimuelekeza Abdul jinsi ya kupiga krosi za katikati ya uwanja na kutosubiria kupiga hadi akifika pembeni kwenye kibendera.
Kocha alionekana kila wakati akimuelekeza beki huyo huku akimsisitiza kabla ya kupiga krosi hizo anatakiwa awaangalie washambuliaji wake walipo ili waweze kufunga kwa faida ya timu.
Alipoulizwa Abdul kuzungumza hilo alisema: “Kila siku najifunza na ninaendelea kujifunza vitu vipya ninavyovipata kutoka kwa makocha wangu.
“Ninafurahi kujifunza kiukweli na kikubwa alikuwa akinipa mbinu mbalimbali za ndani ya uwanja,”alisema Abdul.