Balozi wa Nyumba 10 katika Kitongoji cha Chang’ombe Kijiji cha Chamwino Ikulu, Simango Asheri amesema alishuhudia mwili wa Mariam Said (17) anayedaiwa kuuawa nyumbani kwa mganga wa kienyeji, Ashura Mkasanga (33) ukiwa utupu, umetenganishwa kichwa na kiwiliwili huku ukiungua moto kichwani.
Mauaji hayo yalitokea Agosti 8 mwaka huu saa 10 usiku, umbali wa kilometa mbili kutoka mahali ilipo Ikulu ya Chamwino mkoani hapa.
Akizungumza nyumbani kwake hivi karibuni Asheri alisema wakati akiwa anafanya shughuli zake za ujenzi nyumbani kwake saa 3 asubuhi alipita mwenyekiti wa tawi la CCM akamweleza kuhusu tukio hilo.
“Akaniambia kuna mtu kafa kwa Malita Mkasanga (Ashura), tukakimbia (kwenda) mwenzangu alikuwa na baiskeli mimi nilikuwa peku, tukafika tukakutana na wazee wamekaa tukakaribishwa nendeni mkaangalie tukio,” anasema.
“Tulipofika ndani tukakuta mtu amelala chali sebuleni kuangalia tukaona moto unaendelea kufuka kichwani, alikuwa hana nguo, tulitoka lakini baada ya muda tuliingia tena kutazama tukakuta shingo imesogezwa kwa kukatwa,” anasema.
Balozi huyo anasema walipomuuliza Ashura ilikuaje hadi mtu huyo akafia nyumbani kwake, aliwaambia kuwa akiwa amelala ndani mtoto wake wa kiume alisikia kelele nje.
“Alituambia kuwa marehemu alipiga mlango na kuingia ndani na kudondoka sebuleni huku moto ukaendelea kuwaka, tuliendelea kumuhoji kama mlango uliokuwa umefungwa aliupiga na kuingia ndani mbona ni mzima haukuvunjika, alijibu hata yeye anashangaa,” anasema.
Alipobanwa na wazee wa kijiji kuhusu ni wapi majivu yaliyokuwa ndani ya nyumba hiyo yalipotokea, aliwajibu kuwa hata yeye anashangaa kwa sababu hajui yalipotoka.
“Alipoulizwa kuhusiana na mchanga uliokuwepo ndani ya nyumba hiyo, pia alijibu anashangaa ulipotokea. Kutokana na majibu hayo tulimwacha tukiwasubiri polisi waje,” anasema.
Asheri anasema kuwa pembeni mwa mwili wa marehemu kulikuwa na lundo la mchanga ambalo baada ya kufukuliwa ilibainika kuwa chini kulikuwa na damu iliyofukiwa.
Uhalali wa kazi ya mganga
Hata hivyo, balozi huyo anapoulizwa iwapo alikuwa anafahamu kuwa Ashura alikuwa mganga wa kienyeji, anasema hafahamu na kwamba watu wanaofanya shughuli hizo kijijini hapo wote wanajulikana.
“Wanasema kuwa ni mganga, lakini mimi tangu amehamia hapa miaka mitano hivi namfahamu kama mkulima na mumewe anafanya kazi katika gari moja la kusombea mchanga huko,” anasema.
Badala yake anasema kuwa Ashura alikuwa akishiriki vizuri shughuli za jamii yake kwa kuchanga michango mbalimbali na kushiriki kwenye mikutano ya kitongoji na kijiji.
Ndugu wachukua watoto
Mjomba wa mumewe wa mganga huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anasema baada ya tukio hilo polisi waliwachukua watu wote waliokuwepo ndani ya nyumba hiyo wakiwemo watoto.
“Lakini baadaye tuliambiwa kuwa watoto wameachiwa wamerudi nyumbani, tukaamua twende tukawachukue ili ndugu wa marehemu wasije wakawadhuru,” anasema.
Anasema watoto hao walipelekwa kwa bibi yao na wataishi huko hadi wazazi wao watakapomaliza matatizo yaliyojitokeza.
“Huyu ndugu yetu awali alikuwa akiishi na dada yangu, lakini walikuwa hawaelewani kwasababu mama yake alikuwa akimwambia aachane naye kwasababu ni mshirikina lakini alikataa,” anasema.
Anaongeza kuwa baada ya muda walinunua shamba na hivyo kuondoka kwa mama yake na kwenda kuanzisha mji wao.
Hata hivyo, mmoja wa watoto wa mganga huyo, (jina tunalihifadhi), anasema kuwa siku ya tukio hakulala nyumbani.
“Niliporudi nyumbani asubuhi ndiyo nilikutana na tukio hilo wala sikufahamu ilikuaje,” anasema mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika moja ya shule wilayani humo.
Nyumbani kwa mganga
Mazingira ya nyumba hiyo ambayo ipo umbali wa takriban mita 300 kutoka kwa majirani zake, yamegubikwa na utulivu mkubwa huku milango ikiwa imefungwa.
Nje ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa matofali ya udongo kuna kisima kilichochimbwa kienyeji kikiwa na maji machache, mabua ya mtama uliovunwa na pembeni kukiwa na nyumba iliyoanza kujengwa kwa matofali ya saruji.
Inaelezwa kuwa katika nyumba ya jirani kuna mzee anaishi lakini hata hivyo wakati mwandishi wa habari hizi
anafika hakukuwa na mtu.
Hata hivyo, tofauti na matukio mengine hakuna kiongozi wa kijiji hicho cha Chamwino Ikulu aliyekuwa tayari kuelezea tukio hilo kwa sababu mbalimbali.
Waganga wazungumza
Akizungumza hivi karibuni mmoja wa waganga wa tiba asilia mjini hapa, Dk Harun Kifimbo anasema Serikali ihakikishe mipango inayopangwa kudhibiti watu wanaojifanya waganga wa tiba asilia inasimamiwa.
“Tatizo pia liko kwa baadhi ya waratibu wanaotoa vyeti kwa waganga wasiostahili na ndiyo wanaofanya mambo haya ambayo yanaenda kinyume na tiba ya asili,” anasema Kifimbo.
Anasema chama cha waganga wa tiba asili mkoani Dodoma kimepanga kuendesha msako na kuwakamata watu wanaojishughulisha na tiba hizo bila kuwa na leseni, cheti cha kuthibitishwa mahali wanapofanyia kazi zao na dawa zao kutokuwa na usajili kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, anawalamu baadhi ya waganga kuwa wamekuwa wakijiharibia mambo yao wenyewe kwa kufanya mambo ambayo yanakatazwa kisheria wakati Serikali imewawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa ambaye sasa amehamishiwa Dar es Salaam, alisema waliwakamata watuhumiwa 11 na kuwahoji, kati yao watano wanaendelea kuwa chini ya ulinzi.
“Kule Chamwino wanamamlaka ya kuwafikisha mahakamani wakimaliza uchunguzi wao,” anasema.
Mambosasa alisema jumla ya watu 11 walikamatwa katika tukio hilo ambalo Mariam aliuawa kwa kukatwa shingo yake na kutenganishwa na kiwiliwili na kuchomwa moto kichwa chake na kubakia vufu lisiloweza kutambuliwa sura yake.
“Baadhi ya sehemu za mwili wake ziliunguzwa kwa moto ambazo ni mkono wa kushoto, shingo, kifuani na sehemu za siri,” alisema.
Alisema mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa mganga huyo asiyekuwa na kibali cha kuendesha shughuli za tiba asili analaza wagonjwa nyumbani kwake, anafanya matambiko, anapiga ramli chonganishi na anafanya tohara.
“Katika nyumba yake alikutwa kalaza watu wanane kati yao wanawake sita na wanaume wawili,” anasema.
Hata hivyo, anasema hakuna maelezo ya kutosha jinsi gani marehemu alifika kijijini hapo kutoka Kigoma na kwamba polisi inafanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
“Tukio hili halikubaliki hapa Dodoma na mahali popote ni fedheha kubwa sana kwa wanachamwino kuendelea kukumbatia ushirikina katika karne hii na Serikali imesogeza huduma za afya karibu na jamii, lakini bado hawataki kwenda kutibiwa hospitali na kukubali kuuawa kwa fedheha na waganga wachonganishi wa jadi,” anasema.