Hospitali ya Muhimbili Imezindua Mwongozo Huduma kwa Watoto

Hospitali ya Muhimbili Imezindua Mwongozo Huduma kwa Watoto
Kitengo cha watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kimezindua mwongozo wa kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku 0 hadi 28.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo, daktari wa magonjwa ya watoto ambaye ni mkuu wa kitengo cha watoto wachanga, Edna Majaliwa amesema mwongozo huo ni kwa ajili ya kuwahudumia katika magonjwa mbalimbali na hasa kwa watoto njiti.

"Hii ni hospitali ya rufaa, tunahitaji mwongozo ambao unafanana ili  kuwasaidia wanaoleta wagonjwa kwetu, wajue wanafanya nini kabla na pia tabibu yeyote atakayekuja aweze kumhudumia mtoto hata kabla ya kupata mafunzo upya," amesema.

Dk Majaliwa amesema kwa kipindi kirefu Muhimbili imekuwa ikifanya kazi na madaktari kutoka hospitali mbalimbali, hivyo wakati wa kutengeneza mwongozo huo waliwashirikisha.

Ametoa wito kwa wajawazito kuhakikisha wanafika kliniki  wanapogundua kuwa na ujauzito ili kupunguza ongezeko la watoto njiti wanaolazwa katika kitengo hicho.

"Wakiwahi watagundulika mapema kuwa na viashiria na watafanyiwa matibabu mapema, hata hivyo ni muhimu mama kufika kliniki mara moja kama atagundua kuwa na magonjwa ya mfumo wa mkojo -UTI, presha, upungufu wa damu, kifafa cha mimba, upungufu wa madini na wakiwa pacha ni rahisi kupata mtoto njiti," amesema.

Dk Majaliwa amesema wodi hizo hulaza watoto kati ya 100 na 120.

Amesema kwa kipindi cha Desemba hadi Mei hulaza kati ya watoto 200 na 250 kwa siku.

Akizungumzia takwimu za magonjwa ya watoto wachanga Dk Judith Cosmas wa hospitali hiyo amesema sababu kubwa ni kuzaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito, kushindwa kupumua vizuri, maambukizi baada ya kuzaliwa siku saba za kwanza, wale wanaokuwa na majeraha waliyoyapata wakati wa kuzaliwa na waliozaliwa kwa njia ya upasuaji.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru amesema mwongozo huo utasaidia wataalamu katika kutoa tiba na utatumika kwa waliohitimu pekee.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad