Jaji Mkuu Aliyefuta Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Kenya Atua nchini,

Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga ametua nchini katika mkutano wa majaji na mahakimu akionekana kivutio kwa wengine.

Jaji huyo ni mmoja wa majaji wakuu 13 kutoka nchi mbalimbali duniani wanaohudhuria mkutano majaji na mahakimu wa nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu..

Maraga amegeuka kivutio baada ya kushangiliwa na majaji waliohudhuria mkutano huo wakati alipotambulishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Profesa Juma amempongeza Maraga kwa kuwakilisha mfano bora wa kulinda uhuru wa Mahakama kwa nchi nyingine duniani.

Kiongozi huyo ameonekana akiwa ameambatana na walinzi wanne ambao wanamfuata popote anapotembea nje ya mkutano huo.

Hata hivyo, Maraga amekataa kuzungumza na vyombo vya habari kwa madai amekuja kuhudhuria mkutano huo na siyo kwa jambo jingine lolote.

Mkutano huo umefunguliwa leo Jumatatu na Makamu wa Rais, Samia Suluhu ukiwa na kauli mbiu "Kujenga Mahakama Shirikishi, Thabiti na Inayowajibika."

Jaji Mkuu Aliyefuta Matokeo ya  Uchaguzi Mkuu Kenya Atua nchini,
Jaji Maraga kwa siku za hivi karibuni amekuwa maarufu baada ya kutoa uamuzi wa kufuta Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliokuwa umempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.

Katika mkutano huo Samia amesema rushwa ni kitu ambacho kinaondoa uhuru wa Mahakama na utawala wa sheria katika nchi mbalimbali duniani.

Samia amesema Tanzania inachukua hatua dhidi ya rushwa ili kuhakikisha kwamba Mahakama inatenda haki.

Amesema majaji na mahakimu wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha Mahakama inakuwa uhuru kwa kuzingatia maadili ya kazi yao.

"Mahakama ya Tanzania itahakikisha kwamba rushwa haitakuwa sehemu ya utendaji wake. Tumetangaza vita dhidi ya rushwa katika ngazi zote za Serikali," amesema Samia.

Kiongozi huyo wa Serikali amebainisha changamoto kubwa inayozikabili nchi mbalimbali duniani kuwa ni uhaba wa fedha za uendeshaji wa Mahakama, jambo ambalo linaathiri mifumo ya utoaji haki.

Kwa kutambua hilo, amesema Serikali inajitahidi kuongeza bajeti ya Mahakama kila mwaka wa fedha ili kesi ziamuliwe kwa haraka na kwa haki.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema bajeti ya Mahakama imeongezeka kwa asilimia 100 na wameanza kutekeleza mipango mbalimbali ya kuboresha utendaji.

Profesa Juma amefafanua kwamba katika mpango wa Taifa wa miaka mitano, Mahakama utakaokamilika 2020, zitajengwa mahakama 48 za wilaya, mahakama 100 za mwanzo na mahakama kuu 13 katika sehemu mbalimbali nchini.



"Bajeti inayokidhi mahitaji ni muhimu sana kwa uhuru wa mahakama. Tumekuwa na changamoto ya uhaba wa majengo ya mahakama lakini tunaendea kukabiliana nalo," amesema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad