Mwanamke mmoja nchini Marekani Eva Echeverria, mwenye miaka 63 ameshinda kesi ya madai dhidi ya kampuni ya Johnson & Johnson baada ya kusema kwamba amepata saratani/kansa ya kizazi baada ya kutumia poda ya Johnson’s Baby.
Hukumu hiyo inayomzawadia dola za Kimarekani milioni 417 (dola 1 ni zaidi ya Tsh 2,200) mwanamke huyo ambaye amekuwa akipaka poda hiyo kwa miongo kadhaa imewashtua wengi ambao bado wamekuwa wakiitumia bidhaa hii.
Mwanamke huyo anadai kwamba amepata saratani/kansa ya Ovari baada ya kutumia poda hiyo katika sehemu zake za siri kwa miaka mingi, ingawa hukumu hii haina maana ya moja kwa moja kwamba poda hizi ndiyo chanzo kikuu cha kansa hiyo lakini ushindi katika shauri hili unaamsha hali ya tahadhari kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
Sehemu mbaya kwa kampuni hiyo ni kwamba moja ya ushahidi uliotumiwa na wanasheria wa bibi Eva ni memo ya ndani ya kampuni hiyo ambapo wanasayansi wake walidai ya kwamba kukataa ya kwamba marighafu inaweza kuleta kansa ya kizazi kwa wanawake ni sawa na mtu anayekataa ya kwamba uvutaji sigara unaweza sababisha kansa ya koo/mapafu.
Kwa wanawake inabidi kuwa makini katika utumiaji wa poda hii sehemu za siri. Madai makubwa ni kwamba kuna marighafi muhimu ya poda inayotumika, kama ikifanikiwa kuingia ukeni kwa wingi na kwa muda mrefu inaweza kuleta saratani ya kizazi (Ovari)
Mtandao wa TFDA mamlaka ambayo inahusika na madawa na vyakula kwa Tanzania bado haujatoa taarifa yeyote juu ya hili na pengine baada ya muda watautaarifu umma kama wataona kuna haja hiyo, kikuu ni kwamba bado ata Marekani kwenyewe hili jambo halijapata msimamo rasmi wa kisayansi. Wengi wanaamini utafiti zaidi unatakiwa kuendelea.