Jeshi La Polisi Laamua Kumjibu Lema Lakanusha Kuwakamata Watu Waliovaa T-shirt za Lissu

Jeshi La Polisi Laamua Kumjibu Lema Lakanusha Kuwakamata Watu Waliovaa T-shirt za Lissu
Jeshi la Polisi limemjibu Mbunge Godbless Lema na kusema hakuna mtuhumiwa ambaye amekamatwa na polisi kwa kuvaa Tshirt za CHADEMA wala za Tundu Lissu na kudai watu watatu waliokamatwa Septemba 17, 2017 walifanya makosa ya kukusanyika bila kibali.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amedai kuwa hakuna watu wowote ambao wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kuvaa Tshirt bali walikuwa wanawashikilia watu ambao walikuwa wamefanya uhalifu. Mambosasa amesema hayo siku moja baada ya Mbunge Godbless Lema kupitia mitandao ya kijamii kumuomba IGP Sirro na Waziri Mwigulu Nchemba kuwaachia watu waliokamatwa na polisi kwa kuvaa Tshirt za UKUTA pamoja za Tshirt za 'Pray for Tundu Lissu'

"Hatuna mshtakiwa anaitwa CHADEMA, hatuna mshtakiwa anashtakiwa kwa kuvaa Tshirt ya chama chochote sisi tunachofanya ni kukamata wahalifu wanaotenda makosa ya kijinai, washtakiwa wote wanaokamatwa wanakuwa na mashati, watu wanaokamatwa wanakamatwa kwa kufanya makosa ya jinai, tukikamata mhalifu usiniambie kwamba huyu mhalifu ni CHADEMA mimi hiyo hainihusu" alisema Mambosasa

Aidha Kamanda Mambosasa amesema kuwa vijana watatu ambao walikuwa wamekamatwa kwa kufanya mkusanyiko pasipokuwa na kibali kwa sasa wameachiwa huru kwa kupata dhamana kwani kosa walilotenda ni kosa ambalo linadhamana.

"Walikamatwa watu watatu na walikamatwa kwa kukusanyika kinyume na sheria, nilisimama hapa na nikatoa onyo ni marufuku watu kujikusanya kwa makundi bila ya kibali kwa kisingizio cha kwenda kufanya maombi nikaruhusu watu kwenda kufanya maombi kanisani, misikitini hata wapagani kuna mawe makubwa makubwa nje ya mji wangeenda kuabudu huko, lakini wao walikaidi na walivyoona magari ya polisi walianza kukimbia, na ukianza kukimbia kwamba unanipa mrejesho kwamba unajua ulichotenda kwamba ni kosa ndiyo maana unakimbia" alisema Mambosasa

Aidha Mambosasa anasema kesi ya watu hao kwa sasa inakamilishwa upelelezi na pindi upelelezi utakapokamilika basi watafikishwa mahakamani kwa makosa ambayo wametenda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad